NEWS

Monday 20 March 2023

RPC Tarime Rorya: Mfanyakazi mgodi wa Barrick North Mara hakufa kwa kupigwa risasi, alijirusha shimoni



Na Mara Online News
--------------------------------

KAMANDA wa Polisi Mkoa (RPC) wa Polisi Tarime Rorya, ACP Geofrey Sarakikya (pichani) amesema mfanyakazi wa mgodi wa Barrick North Mara, Emmanuel Chacha (26) hakufa kwa kupigwa risasi.

"Maelezo ya watu waliokuwepo kwenye eneo la tukio, na kutokana na matokeo ya uchunguzi wa mwili wa marehemu Emmanuel Chacha - uliofanywa na Daktari katika Hospitali ya Rufaa Bugando Mwanza, kifo chake kimetokana na majeraha yaliyotokana na kujirusha kwenye shimo lenye urefu wa mita 20.

Kamanda Sarakikya ametupilia mbali taarifa zilizosambazwa kwenye mitando ya kijamii zikidi kuwa mfanyakazi huyo aliuawa kwa kupigwa risasi.

"Taarifa zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kifo cha Emmanuel Chacha kilitokana na kupigwa risasi sio za kweli, huu ndio ukweli," RPC Sarakikya amesisitiza leo asubuhi wakati akihitimisha taarifa yake hiyo kwa vyombo vya habari - ambayo Mara Online News imepata nakala yake.

Kamanda huyo wa Polisi ametoa ufafanuzi huo kutimiza ahadi aliyoitoa Machi 12, 2023 kwamba atatoa taarifa kamili ya kifo hicho baada ya kupata majibu ya kidaktari ya uchunguzi wa mwili wa marehemu huyo.

Katika taarifa yake ya awali, alisema kifo hicho kilitokea Machi 11, 2023 katika eneo la Gokona Underground ndani ya mgodi wa Barrick North Mara.

RPC Sarakikya alifafanua kuwa kabla ya kujirusha kwenye shimo, timu ya kikosi kazi ilimkukuta mfanyakazi huyo akiiba mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu ndani ya mgodi huo.

Alibainisha kuwa timu hiyo ya kikosi kazi ilijumuisha afisa madini wa mkoa, maafisa kutoka wa jeshi la Polisi, kitengo cha ulinzi cha mgodi huo na kampuni ya ulinzi ya Nguvu Moja.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages