NEWS

Saturday 11 March 2023

Sekondari ya Angel House yapongezwa kwa kuenzi tamaduni nzuri za KitanzaniaNa Mara Online News
-----------------------------------

SHULE ya Sekondari Angel House iliyopo Gamasara wilayani Tarime imepongezwa kwa ubunifu wa tamasha la kuenzi tamaduni nzuri za Kitanzania, kupitia mashindano ya michezo mbalimbali ya wanafunzi.

Pongezi hizo zilitolewa na Afisa Elimu ya Watu Wazima na Elimu isiyo Rasmi, Milda Lazaro ambaye alimwakilisha Afisa Utamaduni Wilaya kama mgeni rasmi katika tamasha hilo lililofanyika shuleni hapo, jana Machi 10, 2023.

Ilielezwa kuwa lengo la tamasha hilo ni kuendelea kutunza, kulinda na kuenzi mila na tamaduni nzuri za Kitanzania, sambamba na kutoa elimu ya kupiga vita zinazochangia ukatili na unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.


Aidha, Melda aliwapongeza wanafunzi wa shule hiyo kwa ubunifu walioonesha wakati wakielezea dhima ya tamasha hilo, hususan madhara ya mila ya ukeketaji.

“Niwapongeze wanafunzi wa Angel house kwa kile mlichoonesha, ni ubunifu mkubwa sana mmetumia kuwasilisha mawazo yenu,” alisema.

Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Florence Nyamchere alisema tamasha hilo hufanyika shuleni hapo kila mwaka tangu mwaka 2015, ambapo licha ya kutoa elimu juu ya mila na tamaduni mbalimbali, hutoa burudani kwa wanafunzi.


“Tamasha linajumiisha michezo kama kuigiza, nyimbo, uwasilishaji mada, uchezaji wa nyimbo za kitamaduni na za kizazi kipya, hivyo linaburudisha pia,” alisema Mwalimu Florence.

Alifafanua kuwa michezo hiyo hufanyika kwa mashindano ya madarasa na mshindi hupata zawadi ya mbuzi mnyama na kreti za soda, ambapo mwaka huu mshindi aliyejinyakulia zawadi hizo ni wanafunzi wa kidato cha nne.


"Hapa tunao wanafunzi takriban 400 na lengo letu ni kuhakikisha tunatoa elimu kwa jamii nzima juu ya mambo mbalimbali yanayotuzunguka, hivyo kupitia kwa hawa wanafunzi inakuwa rahisi kufikia watu wengi zaidi kwa sababu tuna imani kuwa nao watakwenda kuelimisha jamii inayowazunguka, hususan juu ya suala la ukeketaji kwa watoto wa kike ambalo ndilo dhima kuu ya mwaka huu,” alisema Mwalimu Hezron Mussa wa Shule ya Sekondari Angel house.

Wageni wengine waliohudhuria hafla ya tamasha hilo ni pamoja na Mkuu wa Shule ya Sekondari Tarime, Mwalimu Maro Chenge ambaye aliapongeza wanafunzi na kuwataka kutumia vizuri vipaji vyao kwa faida ya siku za usoni.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages