NEWS

Sunday 12 March 2023

RPC Tarime Rorya: Mfanyakazi mgodi wa North Mara aliyekufa alijirusha shimoni kabla ya mauti kumfika


RPC Tarime Rorya, ACP Geofrey Sarakikya

Na Mara Online News
--------------------------------

JESHI la Polisi limesema mfanyakazi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara aliyefariki dunia ndani ya mgodi huo alijirusha kwenye shimo lenye urefu wa mita takariban 20 baada ya kukutwa akichimba mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu katika shimo la chini ya ardhi (underground) eneo la Gokona.

“Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Tarime ukisubiri kufanyiwa uchunguzi wa kitabibu kubaini chanzo cha kifo chake,” Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Tarime Rorya, ACP Geofrey Sarakikya ameimbia Mara Online News ofisini kwake leo asubuhi.

RPC Sarakikya amemtaja marehemu huyo kuwa ni Emmanuel Chacha (25), mkazi wa kijiji cha Kemakorere wilayani Tarime, Mara.

RPC Sarakikya amesema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 11 jioni ndani ya mgodi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

“Alijirusha kwenye shimo baada kukutwa anaiba mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu, lakini uchunguzi wa mwili utatoa majibu ya chanzo cha kifo,” amesisitiza RPC Sarakikya.

Bado haijafahamika sababu ya mfanyakazi huyo kujirusha kwenye shimo, ingawa RPC Sarakikiya amesema kabla ya kujirusha timu ya kikosi kazi ilimkukuta akiiba mawe yanayodhaniwa kuwa na dhahabu ndani ya shimo hilo.

Kamanda Sarakikya amefafanua kuwa timu hiyo ya kikosi kazi ilijumuisha afisa madini wa mkoa, maafisa kutoka wa jeshi la Polisi, kitengo cha ulinzi cha mgodi huo na kampuni ya ulinzi ya Nguvu Moja.

Hata hivyo RPC Sarakikya amesema atotoa taarifa kamili ya tukio hilo baada ya uchunguzi wa mwili wa marehemu kukamilika.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages