NEWS

Friday 10 March 2023

Waziri Mchengerwa azindua kituo cha habari cha kisasa katika Hifadhi ya Serengeti


Waziri Mchengerwa (wa tatu kulia mbele) akikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kituo cha Habari Serengeti

Na Mwandishi Wetu, Serengeti
-------------------------------------------------

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa leo amezindua Kituo cha Habari cha kisasa katika Hifadhi ya Taifa Serengeti (Serengeti Media Centre) kilichojengwa eneo la Seronera kwa ufadhili wa Serikali ya Korea Kusini kupitia Shirika lake la KOICA.

Katika hotuba yake, Waziri Mchengerwa ameishukuru Serikali ya Korea Kusini kwa ufadhili huo, akisema kituo hicho kitasaidia kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Serengeti na Tanzania kwa ujumla, pamoja na kutoa taarifa zenye ubora kwa wakati kuhusu utalii na shughuli za uhifadhi nchini.

Waziri Mchengerwa akivutiwa kutazama video ya wanyamapori ndni ya Kituo cha Habari Serengeti


Waziri huyo mwenye dhamana ya maliasili na utalii ametumia nafasi hiyo pia kuelekeza Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuongeza jitihada za ulinzi na uhifadhi wa vivutio vya utalii nchini sambamba na kuvitangaza ndani na nje ya nchi.

“Kila mmoja atumie nguvu zake zote kuhifadhi na kutangaza vivutio vilivyopo. Tanzania ni tajiri kwa vivutio kama si ya kwanza duniani,” amesisitiza Waziri Mchengerwa na kuelekeza watumishi wa TANAPA wajengewe uwezo na kuongezewa ujuzi waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Waziri Mchengerwa (katikati waliokaa), Balozi wa Kore nchini Tanzania, Kim Sun Pyo (wa tatu kushoto), Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (wa tatu kulia), Makamishna wa Uhifadhi (waliosimama) na viongozi wengine katika picha ya pamoja.

Nao Balozi wa Korea nchini Tanzania, Kim Sun Pyo na Mkurugenzi Mkazi wa KOICA nchini, Man Shik Shin wamesema ufadhili wa ujenzi wa kituo hicho ni mwendelezo wa misaada mbalimbali inayotolewa na Serikali ya Korea Kusini kwa TANAPA.

“Kituo cha aina hii ni muhimu kwa dunia ya sasa kwa ajili ya kutangaza utalii na uhifadhi,” amesema Balozi Pyo.

Waziri Mchengerwa akikata keki

Awali, Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, William Mwakilema amemueleza Waziri Mchengerwa kuwa ujenzi wa kituo hicho umegharimu Dola za Kimarekani milioni 1.5, na kwamba lengo lake ni kusaidia kufikia lengo la Taifa la kuongeza idadi ya watalii hadi milioni tano kufikia mwaka 2025.

“Pia kituo hiki kitasaidia kushawishi wageni wanaotembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti kuongeza siku za kukaa hifadhini kutoka moja hadi tatu, na hivyo kuongeza pato la Serikali,” amesema Kamishna Mwakilema.

Sehemu ya mbele ya Serengeti Media Centre

Viongozi wengine waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa kituo hicho ni Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt Hassan Abbas, Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini ya TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji, miongoni mwa wengine.

(Picha zore na Mara Online News)

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages