NEWS

Friday 14 April 2023

Ataka wachochezi wakae pembeni walengwa wazungumze na Serikali kutatua mgogoro wa NyanunguNa Mara Online News
----------------------------------

MWENYEKITI wa Kitongoji cha Ngori kilichopo kata ya Nyanungu, wilaya ya Tarime mkoani Mara, Nyamsabi Marwa ameiomba Serikali kufanya mazungumzo ya kutafuta suluhu na wananchi ambao miji na mashamba yao vimeonekana kuingia ndani ya mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti.

Aidha, kiongozi huyo ameeleza kushangazwa na kitendo cha wananchi na viongozi wasio walengwa wa maeneo hayo kuendelea kufanya kile alichokiita uchochezi unaoweza kuwanyima walengwa nafasi ya kusikilizwa na kupata haki zao.

“Walengwa tu ambao ni walalamikaji wazungumze na Serikali, wale ambao siyo walengwa wanachochea, wanaharibia walengwa,” Nyamsabi amesisitiza katika mazungumzo na Mara Online News  leo.

Amebainisha kuwa miji 22 na mashamba 34 ya baadhi ya wakazi wa kitongoji cha Ngori kilichopo kijiji cha Nyandage, vimeonekana kuwa ndani ya hifadhi ya Serengeti baada ya bikoni za mpaka kuwekwa.

Kwa upande mwingine, kiongozi huyo ameeleza kushangazwa pia na watu wachache akiwemo kiongozi wa kisiasa kutoka chama tawala - CCM katani Nyanungu wanaohoji ziara ya wananchi na viongozi waliofanya ziara ya mafunzo katika hifadhi ya Serengeti hivi karibuni, akisema huo nao ni uchochezi wa kuwagawa wananchi wa kata hiyo.

“Waliofanya utalii wa mafunzo ni jambo la kawaida, sasa mtu unahoji… Mbona hata miaka ya nyuma wananchi, wanafunzi walikuwa wanatembelea hifadhi. Huu nao ni uchochezi tu,” amesema Nyamsabi.

Mbali na Ngori, vitongoji vingine vyenye wananchi ambao mashamba na miji yao ‘vimeangukia’ ndani ya hifadhi ya Serengeti baada ya bikoni za mpaka kuweka hivi karibuni ni Nyarususuni na Nyandage vya kijijini Nyandage, Isorya, Giyema na Kwibate vya kijijini Kegonga.

Serikali inaweka bikoni hizo ili kutatua mgogoro wa muda mrefu wa kugombea mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na vijiji vinavyokana nayo upande wa wilaya ya Tarime, vikiwemo Kegonga na Nyandage vya katani Nyanungu.

Kazi ya kuweka bikoni hizo katika vijiji vya Kegonga na Nyandage katani Nyanungu ilikamilika siku chache zilizopita, na inaripotiwa kuendelea kwa amani katika kata jirani za Gorong’a na Kwihancha.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages