NEWS

Tuesday 25 April 2023

Barrick North Mara, Serikali wilayani Tarime waunganisha nguvu maadhimisho Siku ya Malaria DunianiNa Mara Online News
-----------------------------------

KAMPUNI ya Barrick imefadhili na kushirikiana na Serikali kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani mwaka huu, chini ya uratibu wa Kampuni ya RIN inayofanya kazi na Mgodi wa Dhahabu wa North Mara wilayani Tarime.

Maadhimisho hayo yamefanyika kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Nyamongo leo, ambapo Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya, James Yunge ameishukuru na kuipongeza Barrick kwa mchango mkubwa inaoutoa kuboresha huduma ya afya katika vijiji vilivyo jirani na mgodi huo.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Mgeni rasmi akihutubia

Kuhusu Malaria, Yunge ambaye ni Afisa Tarafa ya Ingwe ameiomba Barrick kuendelea kushirikiana na Serikali wilayani Tarime katika juhudi za kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Aidha kiongozi huyo amewahimiza wananchi kuzingatia maelekezo ya wataalamu kuhusu kinga na matibabu ya Malaria, lakini pia kupima ili kujua hali ya afya zao mara kwa mara.


Kwa upande wake Mwakilishi wa Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Nicholaus Mboya amesema kushirikiana na Serikali katika uboreshaji wa huduma za kijamii ikiwemo afya ni mpango endelevu wa Kampuni ya Barrick.

Naye Meneja Mahusiano wa Mgodi huo, Francis Uhadi amesema sekta ya afya ni miongoni mwa mambo wanayoyapa kipaumbele - ndani na nje ya mgodi kwenye jamii inayouzunguka. “Tunatenga shilingi bilioni mbili kila mwaka kwa ajili ya afya,” amesema.

Awali, akisoma risala ya maadhimisho hayo, Kaimu Mganga wa Wilaya ya Tarime, Dkt Amos Manya amesema Halmashauri ya Wilaya ya Tarime inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kupambana na Malaria, ikiwemo kusambaza kwa wananchi na kuhimiza matumizi sahihi ya vyandarua vilivyotiwa dawa.
Dkt Manya akisoma risala

Pia wakati wa maadhimisho hayo, wananchi walipata huduma za vipimo vya magonjwa mbalimbali ikiwemo Malaria bila malipo, huku akinamama wenye watoto na wazee wakigawiwa vyandarua vilivyotiwa dawa.
Huduma za matibabu zikiendelea

Ugawaji wa vyandarua vilivyotiwa dawa

Kikundi cha ngoma ya asili cha Nyakitari kikitumbuiza wakati wa maadhimisho hayo

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Malaria Duniani mwaka huu inasema “Wakati wa kupambana na Malaria ni sasa: Badilika, Wekeza, Tekeleza - Zero Malaria inaanza na mimi”.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages