NEWS

Monday 3 April 2023

CHADEMA walivyofanikiwa kujichomeka na ‘kuteka’ mkutano wa NyanunguNa Mara Online News
-----------------------------------

KATIKA tukio lisilo la kawaida, baadhi ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Jumamosi iliyopita walifanikiwa kujichomeka na ‘kuteka’ mkutano wa hadhara uliohutubiwa na Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (CCM) katika kijiji cha Kegonga katani Nyanungu.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na Mara Online News umebaini kuwa wana-CHADEMA hao walifanikisha ‘mchongo’ wao huo kupitia kwa kiongozi wa kisiasa ngazi ya kata, ambaye pia alionekana kuwapendelea kwa kuwapa nafasi nyingi mkutanoni ili kuzungumzia mgogoro wa mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na vijiji vinavyopakana nayo upande wa Tarime.

“Wananchi wengi walinyoosha mikono lakini wengi waliochaguliwa na kupewa nafasi ya kuzungumza mkutanoni ni wanachama wa CHADEMA, hali hiyo iliwakera sana viongozi wa CCM kata ya Nyanungu, hatujui kwanini alifanya hivyo,” amesema kada wa CCM aliyehudhuria mkutano huo.

Miongoni mwa makada wa CHADEMA waliofanikiwa kupenya na kupendelewa kupewa nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo ni viongozi wa chama hicho cha upinzani ngazi ya kata.

Kiongozi huyo wa kata anayetokana na CCM, anadaiwa kushirikiana kisirisiri na baadhi ya wanachama wa CHADEMA kupotosha suala la uwekaji wa bikoni za mpaka huo.

Ni katika mkutano huo ambapo pia Diwani wa Kata ya Nyanungu kwa tiketi ya CCM, Tiboche Richard alitangazia umma kuwa udiwani wake hauna maana na kwamba chama chake hicho kikitaka atauachia. “Ndugu zangu mimi niliwambia, narudi tena kusema leo kwenye mkutano huu, udiwani wangu hauna maana yoyote, kama ni udiwani wauchukue,” alisema.

Aidha, Tiboche aliwashangaza wengi kwa kauli yake ya kutaka wanyamapori wawekewe vituo vya kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

“Mwaka 2024, 2025 waje waweke vituo pale - nyumbu wajiandikishe, tembo wajiandikishe ili wapige kura,” Tiboche alikaririwa akitamka ‘live’ maneno hayo katika mkutano huo.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages