
Naibu Waziri Mhandisi Maryprisca Mahundi akimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, alipomtembelea ofisini kwake mjini Musoma juzi.
Musoma
-------------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, Desemba 22, 2025 alizungumza na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, kuhusu umuhimu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare kupandishwa hadhi na kuanza kutoa programu za shahada.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Musoma, RC Mtambi alisema chuo hicho kimekuwa na programu za cheti na diploma kwa muda mrefu, hivyo kutokana na mabadiliko yanayoendelea katika sekta mbalimbali nchini, ni muhimu taifa lipate wataalamu wengi wa maendeleo ya jamii ili kutafsiri dhana ya maendeleo kwa wananchi.
“Sasa hivi mambo mengi yanaenda kisayasi na ni muhimu sana kama wataalamu wa maendeleo ya jamii kuwa na ubobevu mkubwa wa kuweza kutafsiri fursa zilizopo katika sekta mbalimbali ili ziweze kuleta tija kwa wananchi,” alisema.
Aliongeza kuwa kwa sasa wananchi wameanza kupambana kupata maendeleo yao, hivyo ni muhimu kuwa na wataalamu wengi wa maendeleo ya jamii watakaowasaidia wananchi kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa kitaifa na kimataifa.
RC Mtambi alisema Wizara ya Maendeleo ya Jamii inagusa maendeleo ya sekta zote za katika jamii, hivyo kuwa na wataalamu wenye elimu ya umahiri na ubobevu ni muhimu, kwani ndio watakaoishauri serikali kuhusiana mwelekeo sahihi wa maendeleo ya taifa.
Kwa upande wake Naibu Waziri MaryPrisca alisema tayari serikali imefikiria kuhusu kukipandisha hadhi Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare na mchakato wake umeanza na unaenda vizuri.
Alisema kama Wizara wanaendelea kulisukuma jambo hilo ili chuo hicho kipandishwe hadhi na kuanza kutoa shahada mbalimbali.
Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mgore Miraji, alisema chuo hicho kwa kina miaka 57 tangu kilipoanzishwa, na muda wote huo kinatoa programu mbalimbali za cheti na diploma.
Mgore alisema chuo hicho kina miundombinu ya kutosha na kama itahitajika kuongeza haitahitaji uwekezaji mkubwa sana ikilinganishwa na kuanzisha chuo kipya, na kikianza kutoa shahada kitawasaidia wanafunzi wanaotoka mkoa wa Mara kupata elimu ya juu jirani na makazi yao.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Alex Mtaki Nyambiti, alisema chuo hicho kikipandishwa hadhi kitaisaidia katika kuchechemua uchumi wa wananchi na kupandisha makusanyo ya manispaa hiyo.
Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare, Paschal Mahinyila, alisema chuo hicho kimeanzisha mchakato wa kujiunga na Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na kwa msaada wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, mchakato huo unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita ijayo.
Mahinyila alisema mchakato huo ukikamilika, chuo hicho kitakuwa sehemu ya Taasisi ya Tengeru na kinatetarajiwa kuanza kutoa shahada mbalimbali za maendeleo ya jamii mwaka wa masomo 2026/2027 na kuboresha miundombinu, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa jengo la utawala, mabweni na madarasa.
Alibainisha kuwa kwa sasa chuo kina wanafunzi 905 (wanaume 313 na wanawake 592) na watumishi 26 walioajiriwa na wa kujitolea watatu.
No comments:
Post a Comment