NEWS

Monday 17 April 2023

Chonchorio alivyochangisha Sh milioni 20, saruji 185 harambee ya ujenzi Msikiti wa Ijumaa Tarime, awaomba wananchi kuunga mkono juhudi za Rais Samia



Na Mwandishi Wetu, Tarime
------------------------------------------

MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Daniel Chonchorio ameongoza harambee ya ujenzi wa Msikiti mpya wa Ijumaa Tarime na kufanikisha kupatikana kwa shilingi zaidi ya milioni 20 zikiwemo fedha taslimu na ahadi, pamoja na vifaa mbalimbali vya ujenzi.

Chonchorio ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi katika harambee hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi wa Chuo cha Ualimu Tarime Ijumaa iliyopita, alichanga shilingi milioni tatu na kuungwa mkono na rafiki zake, akiwemo mfanyabiashara maarufu, Peter Zakaria aliyetoa shilingi milioni tatu.

Rafiki zake wengine waliomuunga mkono katika harambee hiyo na kiasi cha fedha walizochanga kikiwa kwenye mabano ni pamoja na Samwel Zakaria (milioni tatu), Dura (milioni mbili) na Jackson Kangoye (milioni moja).

“vifaa vya ujenzi vilivyopatikana katika harambee hii ni saruji mifuko 185, mchanga tripu 15 na mawe tripu tano,” alisema Chonchorio wakati akitangaza matokeo ya changizo hilo.


Chonchorio ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mara, alisema amedhamiria kuhamasisha na kuchangia maendeleo ya wana-Tarime, ikiwa ni sehemu ya kutekeleza Ilani ya chama hicho tawala na kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kisekta.

Alitumia nafasi hiyo pia kuwaomba viongozi wa dini kumuombea baraka za Mungu yeye na Watanzania kwa ujumla ili waendelee kumuunga mkono Rais Samia katika juhudi hizo.

“Ndugu zangu Waislamu, viongozi wa dini mtuombee tuendelee kumuunga mkono Mama yetu Rais Samia kwa kazi kubwa anazozifanya za maendeleo katika sekta ya elimu, afya na ujenzi wa taiaf letu. Tumkumbuke katika maombi kwa sababu anayo kazi kubwa ya kuingoza nchi hii,” alisema Chonchorio.

Kwa upande wake Sheikh wa Mkoa wa Mara, Msabaha Kassim alimshukuru Chonchorio na wachangiaji wote katika harambee hiyo na kuwaombea mafanikio zaidi katika shughuli zao.

“Mungu atawalipa - aliye chini Mungu amanyanyue, awalinde muendelee na nafasi zenu. Tutawaombea mfanikiwe zaidi katika shughuli zenu, Mungu awafungulie njia zaidi,” alisema Sheikh Msabaha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa wakati wa harambee hiyo, ujenzi wa Msikiti mpya wa Ijumaa Tarime utagharimu shilingi zaidi ya bilioni moja.

Chonchorio (mwenye kanzu nyeupe) na mfanyabiashara maarufu, Peter Zakaria (wa tatu kulia) wakiwa na viongozi wa Kiislamu wakati wa harambee hiyo.

Siku chache kabla ya harambee hiyo, Chonchorio aliandaa hafla ya maandalizi ya Sikukuu ya Pasaka, kubadilishana mawazo na kula chakula cha mchana cha pamoja na wanachama na viongozi wa CCM, iliyofanyika CMG Hotel mjini Tarime.

Katika hafla hiyo, Chonchorio alionesha nia ya kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa vijana na sekta ya elimu Tarime Mjini, ambapo aliahidi kusimamia kwa hali na mali uanzishaji na uendelezaji wa mradi wa matofali wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Jimbo la Tarime Mjini.

Alisema mradi huo wa ufyatuaji na uuzaji wa matofali ya saruji na mchanga unaotarajiwa kuanza Mei mwaka huu, utawezesha vijana hao kuondokana na hali ya utegemezi.

“Mradi huo wa matofali utakuwa na manufaa kwa vijana wetu ili waondokane na utegemezi. Wateja wetu watakuwa ni Serikali na wananchi wa kawaida,” Chonchorio aliuambia mkutano huo.

Alibainisha kuwa uanzishaji wa mradi huo utamgharimu yeye na rafiki zake shilingi milioni 50 na kwamba tayari ameshatoa shilingi milioni tano za maandalizi ya eneo la mradi, ikiwemo ununuzi wa mashine ya kufyatua matofali na kurudisha gharama za mpangaji aliyekuwepo.

Mjumbe huyo wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa aliongeza kuwa ataendelea kuwaomba rafiki zake na wadau mbalimbali wa maendeleo kumsaidia kupiga jeki mradi huo ili uwe mkubwa na kuwainua kiuchumi vijana wengi zaidi.

Katika hatua nyingine, Chonchorio alitumia nafasi ya hafla hiyo pia kufanya changizo la ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika jimbo la Tarime Mjini, ambapo yeye aliahidi kugharimia ujenzi wa kimoja, huku rafiki zake wakiahidi kumuunga mkono kwa kugharimia ujenzi wa viwili.

Wakati Chonchorio akiahidi kugharimia ujenzi wa chumba cha darasa katika Shule ya Msingi Sabasaba, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Kiles na Magwi Itembe waliahidi kugharimia ujenzi wa kimoja kwenye shule mojawapo katani Turwa.

Nao Diwani wa Kata ya Ganyange, Siza Keheta na Samwel Chomete waliahidi kugharimia ujenzi wa chumba cha darasa katika mojawapo wa shule za katani Ketare.

“Ninaahidi kwamba nitajenga darasa zima, Mungu akituweka hai - ndani ya miezi isiyozidi minne nitakabidhi darasa lililokamilika,” alisema Chonchorio.

Alisema yeye kama Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, amedhamiria kwa dhati ya moyo kushirikiana na wanachama na viongozi wengine kuchangia maendeleo ya chama hicho tawala, na kwamba atahakikisha anatimiza ahadi zote alizotoa wakati anaomba nafasi hiyo.

“Ndugu zangu mimi nimewiwa kufanya kazi za chama, mimi ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, hivyo ni sehemu ya majukumu yangu kuhakikisha kwamba ninakutana na wanachama, tunasikiliza kero zao na pale tunapokuwa tumebarikiwa na Mungu tunawasaidia chochote kinachopatikana ili chama chetu kiendelee kuwa imara.

“Kuna ahadi nilizotoa wakati naomba nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, baadhi nimeshatekeleza na nyingine nazikumbuka vizuri sana - ziko pale pale. Sitaki kuwa kiongozi wa kutoa ahadi za uongo, lazima nitazitimiza Mungu akiendelea kutuweka hai,” alisema Chonchorio.

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages