Na Mwandishi Wetu
------------------------------
KAMPUNI ya Mbolea Tanzania (TFC) imewasilisha mbolea ya kukuzia aina ya UREA yenye uzito wa tani 240 (sawa na mifuko 5,400), ikiwa ni ruzuku iliyotolewa na Serikali ili kusambaza kwa wakulima katika wilaya ya Tarime mkoani Mara msimu huu.
Mkurugenzi wa Biashara wa kampuni hiyo ya Serikali, Lameck Borega aliiambia Sauti ya Mara katika mahojiano maalum mjini Tarime juzi kwamba mbolea hiyo iliwasili Ijumaa iliyopita kwenye maghala ya Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Mara (WAMACU Ltd).
“Tumeleta mbolea hii kwa ajili ya kusaidia wakulima waliokuwa wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mbolea ya ruzuku, na kama ilivyo kawaida yetu sisi TFC hatupeleki sehemu za mijini tu - tunapeleka mpaka vituo vya vijijini ili kumfikia mkulima wa mwisho,” alisema Borega.
Alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuhamasisha wakulima kutoka maeneo mbalimbali wilayani Tarime kujitokeza kuchangamkia mbolea hiyo inayouzwa kwa bei elekezi ya shilingi 70,000 kwa kila mfuko wenye uzito wa kilo 50.
“Waje kuchukua mbolea hii ya ruzuku, ikiwa ni mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Mama yetu Samia Suluhu Hassan katika kumuinua mkulima,” alisema.
Hata hivyo Borega alieleza kuridhishwa na idadi kubwa ya wakulima aliowakuta wamejitokeza kununua mbolea hiyo. “Tunaona wakulima wanachangamkia sana mbolea hizi, ni wengi sana wanaonunua mbolea kipindi hiki cha kukuzia,” alisema.
Borega aliweka wazi kuwa Serikali imetoa shilingi zaidi ya bilioni 150 kwa ajili ya kuwezesha wakulima nchini kupata mbolea za kupandia na kukuzia mazao kwa bei nafuu, hasa kipindi hiki ambacho bei ya mbolea imepanda katika soko la dunia.
Lameck Borega
“Kama tunavyojua bei ya mbolea duniani imepanda sana. Mfano mfuko wa kilo moja ya mbolea ya UREA unauzwa kwa takriban shilingi 150,000 kwenye soko la dunia, lakini Serikali yetu kupitia Wizara ya Kilimo imetoa ruzuku ya shilingi zaidi ya bilioni 150 ili kupooza bei ya mbolea kwa wakulima wetu waweze kuipata kwa shilingi 70,000,” alisema Borega.
Alisema TFC itaendelea kuleta mbolea zaidi katika wilaya ya Tarime na mkoa wa Mara kwa jumla ili wakulima wasipate shida ya kulazimika kununua kutoka nchi jirani kwa bei kubwa.
“Tunaishukuru sana Serikali kuiwezesha kampuni ya TFC kupitia Wizara ya Kilimo na viongozi wake, Mheshimiwa Waziri Hussein Bashe, Naibu Waziri wake, Anthony Mavunde pamoja na Katibu Mkuu, Gerald Mweli na Hussein Omar ambaye ni Naibu Katibu Mkuu.
“Hao viongozi wote wanafanya jitihada kubwa sana kwa Serikali yetu inayoongozwa na Mama Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha mkulima anapata mbolea na pembejeo kwa bei ambazo zinavumilika ili kuifikisha ile ajenda ya 1030 ya kilimo biashara,” alisema Borega.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, TFC inajizatiti kutafuta ufumbuzi wa tatizo la ucheleweshaji wa mbolea kwa wakulima kutokana na changamoto za usafirishaji.
“Kuna changamoto chache za hapa na pale katika usafirishaji kwa sababu mbolea inatokea Dar es Salaam, kuisafirisha mpaka Tarime wakati mwingine inachukua muda mrefu, lakini hilo tunakwenda kulitatua,” alisema.
Kuhusu shughuli za uuzaji/ ugawaji mbolea ya ruzuku, Borega alisema utaratibu uliowekwa na Serikali lazima uzingatiwe ili kuepuka usumbufu na kero kwa wakulima.
“Niwaombe viongozi wanaosimamia ugawaji wa mbolea hizi, kila mkulima auziwe mbolea yeye kama yeye, wasiuziwe watu ambao ni madalali, na bahari nzuri wakulima wote wameandikishwa kwenye mfumo wetu wa kompyuta TFRA. Ninaamini kila mkulima ana jina lake, ana namba ya kitambulisho.
“Kwa hiyo tuhakikishe kwamba anayekuja kununua mbolea ni yule mkulima halisi, tusiuzie mtu ‘kati’ anachukua mifuko labda 50 halafu anasogea pembeni anaanza kuwauzia wakulima kwa shilingi 90,000 mpaka 100,000, hilo hatutalivumilia, na ndio maana na mimi mwenyewe nimefika hapa kushuhudia na kuhakikisha wakulima wanapata mbolea kwa bei stahiki.
“Na tumeweka utaratibu mzuri kwamba wale akina mama na wazee tunawapa kipaumbele cha kuingia kwanza wanahudumiwa halafu ndio wanafuata wengine,” anaeleza Borega.
Kwa upande wake Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU Ltd, Samwel Marwa Gisiboye alimshukuru Rais Samia kwa jitihada anazofanya kuhakikisha kuwa wakulima wa mkoani Mara wanapata mbolea za ruzuku.
GM Gisiboye
“Mpaka sasa tumeshapokea tani 990 mbazo ni sawa na mifuko 19,800 ya mbolea za kupandia aina ya DAP na UREA za kukuzia. Mbolea hizi zimeletwa na taasisi mbili; Kampuni ya Serikali ya TFC na Kampuni ya OCP Tanzania Ltd ambayo imeleta tani 660,” alisema GM Gisiboye.
Alisema wakulima mkoani Mara wanaendelea kupata huduma ya kuuziwa mbolea kwa bei elekezi, japokuwa wakati mwingine mahitaji ya mbolea ya kupandia aina ya UREA yanakuwa mengi kuliko inayopatikana.
GM Gisiboye aliendelea kutoa wito wa kuhimiza wakulima kuendelea kujiandikisha kwenye daftari maalum na kupata namba kwa ajili ya kununua mbolea ya ruzuku.
“Wakulima wajisajili kwa wingi ili kupata mbolea hii, hii ni fursa, Serikali imedhamiria kum- support (kumsaidia) mkulima. Mbolea ipo na matumaini yetu ni kwamba itakuwepo mpaka msimu unaofuta,” alisema.
WAMACU Ltd ni miongoni mwa Vyama Vikuu vya Ushirika vilivyopewa dhamana ya kusimamia usambazaji wa mbolea za ruzuku aina ya DAP na UREA kwa wakulima, kwa kushirikiana na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) tangu Novemba mwaka jana.
WAMACU Ltd inajishughulisha na ukusanyaji wa kahawa kutoka kwa wakulima kwa ajili ya kuiongezea thamani na kuitafutia masoko ya nje. Pia kwa sasa ina leseni ya uwakala wa kusambaza pembejeo, ikiwemo mbolea kutoka TFRA.
Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment