NEWS

Sunday 16 April 2023

Vigingi 180 vyawekwa mpaka wa vijiji vya Tarime na Hifadhi ya Serengeti



Na Mara Online News
------------------------------------

TAKRIBAN vigingi 180 vimewekwa kwenye mpaka wa vijiji saba vya wilaya ya Tarime na Hifadhi ya Taifa Serengeti kuwezesha kila upande kuelewa mwisho wa mpaka wake.

Mabali na kuepusha migongano isiyo ya lazima kati ya wahifadhi na wananchi, uwekaji wa vigingi hivyo unaelezwa kuwa utasaidia kuimirisha mahusiano ya ujirani mwema kati ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na vijiji hivyo.

“Lengo la kuweka hivi vigingi ni kuwezesha wananchi kufahamu mpaka wao na hifadhi unaishia wapi,” anasema moja wa wataalamu kutoka Wizara ya Aridhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi - aliyehusika katika kuweka vigingi hivyo.

Hali hiyo inaelezwa kuwa itasaidia kuharakisha maendeleo ya kijamii, kiuchumi na uhifadhi katika vijiji hivyo.

Vijiji hivyo ni Kegonga, Nyandage, Kenyamsabi, Masanga, Karakatonga, Kwihancha na Gibasso.

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa TANAPA imetoa mamilioni ya fedha kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii katika sekta za elimu na afya kwenye baadhi ya vijiji hivyo - kupitia mpango wake wa ujirani mwema.

Taarifa hizo zinaonesha kuwa TANAPA ambayo majukumu yake ni kulinda na kuhifadhi Hifadhi za Taifa nchini, imetoa shilingi milioni 71 kugharimia ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule ya Msingi Kegonga iliyopo kata ya Nyanungu.

Kata ya Nyanungu ina vijiji viwili ambavyo vinapakana na Hifadhi ya Serengeti, ambavyo ni Kegonga na Nyandage.

Mpango wa ujirani mwema wa TANAPA unalenga kuwafikia wananchi waishio jirani na Hifadhi za Taifa kuanzia ngazi ya kijiji, kata, wilaya hadi mkoa ili kuwajengea uelewa na kuwafanya kuwa sehemu ya juhudi zinazofanywa na shirika hilo katika uhifadhi wa maliasili na mazingira.

Wakati huo huo, viongozi wa baadhi ya vitongoji ambavyo wananchi wake wameathiriwa na uwekaji wa vigingi hivyo wameomba kuzungumza na Serikali badala ya kuruhusu kila mtu wakiwemo wanasiasa, wakazi wa vijiji jirani, au nje ya kata ya Nyunungu wanaotaka kuligeuza suala hilo kuwa la kisiasa.

“Walengwa tu ambao ni walalamikaji wazungumze na Serikali, wale ambao siyo walengwa wanachochoea, wanaharibia walengwa,” Mwenyekiti wa Kitongoji cha Ngori, Nyamsabi Marwa aliiambia Mara Online News, juzi.

Nyamsabi alibainisha kuwa miji 22 na mashamba 34 ya baadhi ya wakazi wa kitongoji hicho kilichopo kijijini Nyandage vimeonekana kuwa ndani ya hifadhi ya Serengeti baada ya vigingi vya mpaka kuwekwa.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages