NEWS

Tuesday 11 April 2023

Chonchorio kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa vijana na sekta ya elimu Tarime Mjini


Daniel Chonchorio (katikati)

Na Mwandishi Wetu, Tarime
----------------------------------------

MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Daniel Chonchorio ameahidi kusimamia kwa hali na mali uanzishaji na uendelezaji wa mradi wa matofali wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Jimbo la Tarime Mjini.

Chonchorio aliyasema hayo wakati wa hafla aliyoiandaa ya maandalizi ya Sikukuu ya Pasaka, kubadilishana mawazo na kula chakula cha mchana cha pamoja na wanachama na viongozi wa CCM, iliyofanyika CMG Hotel mjini hapa, juzi.

Alisema mradi huo wa ufyatuaji na uuzaji wa matofali ya saruji na mchanga unaotarajiwa kuanza Mei mwaka huu, utawezesha vijana hao kuondokana na hali ya utegemezi.

“Mradi huo wa matofali utakuwa na manufaa kwa vijana wetu ili waondokane na utegemezi. Wateja wetu watakuwa ni Serikali na wananchi wa kawaida,” Chonchorio aliuambia mkutano huo.

Alibainisha kuwa uanzishaji wa mradi huo utamgharimu yeye na rafiki zake shilingi milioni 50 na kwamba tayari ameshatoa shilingi milioni tano za maandalizi ya eneo la mradi, ikiwemo ununuzi wa mashine ya kufyatua matofali na kurudisha gharama za mpangaji aliyekuwepo.

Chonchorio akisalimia wajumbe wa mkutano huo ukumbini

Mjumbe huyo wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa aliongeza kuwa ataendelea kuwaomba rafiki zake na wadau mbalimbali wa maendeleo kumsaidia kupiga jeki mradi huo ili uwe mkubwa na kuwainua kiuchumi vijana wengi zaidi.

Katika hatua nyingine, Chonchorio alitumia nafasi ya hafla hiyo pia kufanya changizo la ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika jimbo la Tarime Mjini, ambapo yeye aliahidi kugharimia ujenzi wa kimoja, huku rafiki zake wakiahidi kumuunga mkono kwa kugharimia ujenzi wa viwili.

Wakati Chonchorio akiahidi kugharimia ujenzi wa chumba cha darasa katika Shule ya Msingi Sabasaba, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), Simion Kiles na Magwi Itembe waliahidi kugharimia ujenzi wa kimoja kwenye shule mojawapo katani Turwa.

Nao Diwani wa Kata ya Ganyange, Siza Keheta na Samwel Chomete waliahidi kugharimia ujenzi wa chumba cha darasa katika mojawapo wa shule za katani Ketare.

“Ninaahidi kwamba nitajenga darasa zima, Mungu akituweka hai - ndani ya miezi isiyozidi minne nitakabidhi darasa lililokamilika,” alisema Chonchorio.

Chonchorio akizungumza mkutanoni

Chonchorio alisema yeye kama Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, amedhamiria kwa dhati ya moyo kushirikiana na wanachama na viongozi wengine kuchangia maendeleo ya chama hicho tawala, na kwamba atahakikisha anatimiza ahadi zote alizotoa wakati anaomba nafasi hiyo.

“Ndugu zangu mimi nimewiwa kufanya kazi za chama, mimi ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, hivyo ni sehemu ya majukumu yangu kuhakikisha kwamba ninakutana na wanachama, tunasikiliza kero zao na pale tunapokuwa tumebarikiwa na Mungu tunawasaidia chochote kinachopatikana ili chama chetu kiendelee kuwa imara.

“Kuna ahadi nilizotoa wakati naomba nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Taifa, baadhi nimeshatekeleza na nyingine nazikumbuka vizuri sana - ziko pale pale. Sitaki kuwa kiongozi wa kutoa ahadi za uongo, lazima nitazitimiza Mungu akiendelea kutuweka hai,” alisema Chonchorio.

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages