NEWS

Saturday 29 April 2023

Jeshi la Polisi Tarime Rorya laweka hadharani mafanikio ya operesheni zake kwa usalama wa raia na mali zao



Na Mara Online News
----------------------------------

JESHI la Polisi Mkoa wa Polisi Tarime Rorya limeweka hadharani mafanikio mbalimbali ya misako na operesheni zake katika mkoa huo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC), ACP Geofrey Sarakikya (pichani juu katikati) aliwambia waandishi wa habari ofisini kwake jana Ijumaa kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika kubaini, kuzuia, kutanzua na kupunguza hofu ya uhalifu na wahalifu ndani ya mkoa huo kati ya Machi 23 na Aprili 26, 2023.

RPC Sarakikya alifafanua kuwa mafanikio hayo yamejumuisha kukamatwa kwa watuhumiwa wa mauaji, unyang’anyi wa kutumia silaha, wizi wa mifugo na mali nyingine mbalimbali.

Alisema ukamataji umejumuisha watuhumiwa wanne wa mauaji, dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa kilo 142.7, mirungi kilo 35 pamoja na watuhumiwa 16, pikipiki nne na gari vilivyokuwa vinatumika kuzisafirisha.

“Pia tumefanikiwa kukamata gongo lita 218.5 pamoja na watuhumiwa 43 wakiwemo wauzaji na watumiaji wa pombe hiyo na watafikishwa mahakamani,” aliongeza RPC Sarakikya.

Aidha, alitaja mali za wizi zilizokamatwa kuwa ni pikipiki tatu, cherehani moja, redio, simu janja, betri, runinga, sala moja na watuhumiwa tisa kuhusiana na wizi huo.

Kamanda Sarakikya alisema pia ng’ombe sita na kondoo mmoja vimeokolewa katika wilaya za kipolisi za Tarime, Sirari na Shirati na watuhumiwa sita wamekamatwa kuhusiana na wizi wa mifugo hiyo.

Alisema idadi ya makosa ya usalama barabara yaliyokamatwa kutokana na operesheni na kaguzi kwenye vyombo mbalimbali vya moto ni 2,159.

Lakini pia alisema jeshi hilo limesimamia kesi za washtakiwa wa mauaji hadi mahakama ikahukumu mmoja kunyongwa hadi kufa, mmoja wa unyang’anyi wa kutumia nguvu kufungwa miaka 30, wanne miaka 30 jela kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa ulawiti na utoroshaji wanafunzi na mwingine kifungo cha maisha kwa makosa ya ukatili wa kijinsia na ubakaji na

“Pamoja na mafanikio hayo, Jeshi linaendelea kushirikisha jamii katika kutoa elimu kupitia vyombo vya habari, mazoezi ya pamoja na tumeweza kufanya mikutano 147 na vikao 16 kuelimisha jamii kuhusu masuala ya ulinzi na usalama pamoja na ukatili wa kijinsia kwa watoto,” alieleza RPC huyo.

Alitaja makundi ya wananchi yaliofikiwa na elimu hiyo kuwa ni pamoja na wendesha pikipiki na bajaj, abiria, viongozi wa makundi ya vijana, wazee, walemavu, wajumbe wa kamati za serikali za vijiji na kata, wavuvi, wafanyabiashara ya mifugo na wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.

“Jeshi linaahidi kuendelea kutunza siri za watoa taarifa watakaosaidia kuzuia uhalifu na kuwezesha kukamatwa kwa wahalifu, na tunawasihi wananchi wema kuendelea kutoa taarifa fiche ili kuimarisha ulinzi na usalama katika mkoa wetu,” alihitimisha RPC Sarakikya.

#Tunakuhabrisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages