NEWS

Wednesday 5 April 2023

Mbunge Muhongo awashika mkono waathirika wa mafuriko Musoma Vijijini


Mbunge wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo (mwenye fulana nyeupe) akigawa msaada wa mahindi kwa wananchi walioathiriwa na mafuriko kijijini Kusenyi.

Na Mara Online News
-----------------------------------

MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo, ametembelea kijiji cha Kusenyi katika kata ya Suguti na kutoa pole kwa wananchi walioathiriwa na mafuriko.

Katika ziara yake hiyo ya jana, Prof Muhongo alishuhudia uharibifu uliotokana na mafuriko hayo, sambamba na kugawa msaada wa chakula kwa waathirika wa janga hilo.

Msaada huo wa chakula ulihusisha mahindi magunia 25 mahindi (kila moja likiwa na uzito wa kilo 108) na maharage kilo 100.

Vitongoji vilivyoathirika zaidi kutokana na mafuriko hayo ni Nyabweke chenye kaya 26 na Kwikuyu chenye kaya 24.

“Wakati tathmini ya uharibifu uliotokana na mafuriko hayo ikiendelea kufanywa, Mbunge Muhongo amebaini kuwa baadhi ya nyumba zimebomoka na kuanguka,” imeeleza taarifa iliyotolewa na ofisi ya Mbunge wa Musoma Vijijini.

Pia imebainika kuwa baadhi ya nyumba zimepasuka nyufa kiasi cha kutofaa kutumika tena na chakula kilichotunzwa majumbani katika baadhi ya kaya kimeharibika na kingine kusombwa na maji.

“Kuku na bata wamesombwa na maji, tope ni nyingi sehemu za makazi ya watu,” imeongeza sehemu ya taarifa hiyo.

Prof Muhongo (mwenye fulana nyeupe) akishuhudia uharibifu wa makazi ya watu uliosababishwa na mafuriko kijijini Kusenyi.

Imeelezwa kwamba maafa hayo yamechangiwa na ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita tano ambao haukuzingatia uwekaji wa njia za kutosha kupitisha maji kwenda Ziwa Victoria.

“Wakulima wa mpunga walioko sehemu ya juu ya kijiji cha Kusenyi wameweka miundombinu yao ya kilimo inayozuia maji kutitirika kwenye mikondo inayoelekea ziwani,” taarifa hiyo imeongeza.

Bado waathirika wa mafuriko hayo kutoka kijijini Kusenyi wanahitaji misaada ya chakula, vifaa vya ujenzi na ujenzi wa miundombinu mikubwa ya kutiririsha maji kwenda ziwani.

Mbunge Muhongo anaomba michango yote kutoka kwa wasamaria wema iwasilishwe kwenye ofisi ya Mkuu Wa Wilaya ya Musoma (+255 756 088 624).

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages