NEWS

Sunday 2 April 2023

Mbunge wa CCM aipinga Serikali uwekaji wa bikoni Nyanungu, Diwani Tiboche akitisha chama hicho tawala


Mbunge Waitara akihutubia mkutano wa hadhara kijijini Kegonga jana

Na Mara Online News
------------------------------------

MBUNGE wa Tarime Vijijini kupitia chama tawala - CCM, Mwita Waitara ametangaza kutounga mkono uwekaji wa bikoni (vigingi) unaotekelezwa na Serikali katika vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti upande wa jimbo hilo.

Akihutubia mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kegonga katani Nyanungu jana baada ya kutembelea maeneo yaliyowekwa bikoni, Mbunge Waitara (pichani juu) alidai mpango huo ni haramu na kuwataka wananchi kuendelea kuyatumia kwa kilimo.

“Yale mashamba ya watu, wananchi waendelee kulima kama kawaida. Zile bikoni siyo halali ni ‘fake’… wanatulazimisha kwenda wanakotaka,”Waitara ambaye amewahi kuhudumu kama Naibu Waziri kwenye wizara mbalimbali katika Serikali ya Awamu ya Tano na Sita aliwambia wananchi hao.

Alisisitiza kutounga mkono uwekaji wa bikoni hizo akidai wanavijiji husika hawakushirikishwa katika maridhiano ya kutekeleza mpango huo.

Naye Diwani wa Kata ya Nyanungu kwa tiketi ya CCM pia, Tiboche Richard akizungumza awali katika mkutano huo, alipinga uwekaji wa bikoni hizo akitoa sababu kama hizo za Mbunge Waitara.
Diwani Tiboche akizungumza mkutanoni

Tiboche alikwenda mbali zaidi na kusema udiwani wake hauna maana na kwamba chama chake kikitaka atauachia. “Ndugu zangu mimi niliwambia, narudi tena kusema leo kwenye mkutano huu, udiwani wangu hauna maana yoyote, kama ni udiwani wauchukue,” alisema.

Msimamo huo wa Mbunge Waitara na Diwani Tiboche unatofautiana na viongozi wao chama tawala ngazi ya wilaya na mkoa, ambao wanaunga mkono uwekeji wa vigingi hivyo ili kupata suluhu ya mgogoro uliopo.

Hivi karibuni, Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Valentine Maganga aliwataka wananchi wa kata ya Nyanungu kuendelea kuwa watulivu kipindi hiki cha uwekaji wa vigingi vya mpaka wa vijiji vyao na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, huku akiwatia moyo kuwa Serikali ya chama hicho tawala iko makini kuhakisha maslahi yao yanazingatiwa.

Akizindua uwekaji wa vigingi hivyo Machi 27, 2023, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee alitoa onyo kwa wanasiasa wanaochonganisha wananchi na Serikali ili kukwamisha shughuli hiyo. “Nawaonya… msijione mko juu ya sheria,” alisisitiza.

Serikali inatekeleza mpango wa kuweka bikoni ili kutatua mgogoro wa muda mrefu wa kugombea mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vijiji vinavyopakana nayo upande wa wilaya ya Tarime, vikiwemo Kegonga na Nyandage vya katani Nyanungu.

Taarifa zaidi kutoka serikalini zinasema uwekaji wa vigingi hivyo ni utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kutokana na ushauri wa Kamati ya Mawaziri Wanane wa Kisekta iliyoundwa na Serikali kukusanya maoni ya ufumbuzi wa migogoro ya ardhi kati ya wananchi na Hifadhi za Taifa nchini, ikiwemo Serengeti.

Hata hivyo hadi Ijumaa ya wiki hii, kazi ya uwekaji wa vigingi vya mpaka wa vijiji vya katani Nyanungu na Hifadhi ya Serengeti iliripotiwa kuedeleea kwa amani, huku baadhi ya wananchi wa maeneo hayo wakijitokeza kutoa ushirikiano. Kazi hiyo ya kuweka vigingi inatekelezwa na wataalamu wa Serikali kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages