NEWS

Monday 24 April 2023

Polisi wasema idadi ya waliopoteza maisha katika ibada ya ‘kufunga hadi kufa’ nchini Kenya imefikia 58POLISI wamefukua miili 58 kutoka kwenye makaburi ya halaiki katika msitu wa Shakahola, Mashariki mwa Kenya, inayodhaniwa kuwa wafuasi wa madhehebu ya Kikristo walioamini kwamba wangeenda mbinguni ikiwa wamefunga.

Moja ya makaburi hayo inaaminika kuwa na miili ya watu watano wa familia moja, yaani watoto watatu na wazazi wao, amesema Mkuu wa Polisi wa Kenya.

Idadi ya waliofariki, ambayo imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika muda wa siku mbili zilizopita huku uchimbuaji ukifanywa, inaweza kuongezeka zaidi kwani Shirika la Msalaba Mwekundu la Kenya limesema watu 112 wameripotiwa kupotea kwenye dawati la ufuatiliaji wanaloendesha.

Ibada hiyo iliitwa Good News International Church na kiongozi wake, Paul Mackenzie, alikamatwa kufuatia taarifa iliyodokeza kuwapo kwa makaburi yenye kina kirefu yenye miili ya wafuasi wake 31.

Polisi walisema uchimbuaji wa makaburi mengine ili kutafuta miili zaidi unaendelea.
Kiongozi wa kanisa hilo, Paul Makenzie Nthenge yuko rumande, akisubiri kufikishwa mahakamani. Shirika la utangazaji la KBC lilimtaja kama "kiongozi wa ibada".

Kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa mhubiri huyo mwenye utata, ambaye aliwataka wafuasi wake kufunga hadi kufa, ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Kenya, William Ruto ambaye amemtaja mhubiri huyo kuwa gaidi.

Nthenge amekana kutenda makosa, lakini amenyimwa dhamana. Anasisitiza kwamba alifunga kanisa lake mwaka 2019.

Inadaiwa aliwambia wafuasi wajinyime kwa njaa ili "kukutana na Yesu".

Gazeti la kila siku la Kenya, The Standard, lilisema wataalamu wa magonjwa watachukua sampuli za DNA na kufanya vipimo ili kubaini iwapo watu hao walikufa kwa njaa.

Victor Kaudo wa Kituo cha Haki za Kijamii cha Malindi aliambia Citizen TV "tunapokuwa kwenye msitu huu na kufika katika eneo ambalo tunaona msalaba mkubwa na mrefu, tunajua hiyo inamaanisha zaidi ya watu watano wamezikwa humo".

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya, Kithure Kindiki, alisema ekari zote 800 za msitu huo zimefungiwa na kutangazwa kuwa eneo la uhalifu.

Nthenge alidaiwa kuvipa majina vijiji vitatu vya Nazareti, Bethlehemu na Yudea na kuwabatiza wafuasi kwenye madimbwi kabla ya kuwambia wafunge, gazeti la The Standard linaripoti.

Kenya ni nchi ya kidini na kumekuwa na visa vya hapo awali vya watu kuvutiwa katika makanisa hatari, yasiyodhibitiwa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages