NEWS

Monday, 24 April 2023

Miradi mipya 54 ya CSR Barrick North Mara yakamilika Tarime Vijijini, DED Shati asema imekidhi thamani ya fedha


Mtaalamu akikagua mradi wa chumba cha darasa uliokamilika

Na Mwandishi Maalumu
----------------------------------

MIRADI mipya zaidi ya 50 imetekelezwa na kukamilika kwa asilimia 100 katika vijiji mbalimbali vya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini), chini ya mpango wa Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR) wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara.

“Miradi 54 ya CSR kutoka Barrick North Mara imekamilika kwa silimia 100, kati ya hiyo, 53 ni mipya na mmoja ulikuwa kiporo cha ukamilishaji wa barabara ya lami katika mji wa Nyamongo,” Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Tarime, Solomon Shati aliiambia Sauti ya Mara ofisini kwake, juzi.

Sekta ya elimu inaongoza kwa kuwa na miradi mingi iliyokamilika - ikifuatiwa na afya, kwa mujibu wa DED Shati.

Anafafanua kuwa miradi ya elimu iliyokamilika ni 40, afya 12, maji mmoja na barababara mmoja, yote ikiwa imegharimu shilingi bilioni 3.2 za mpango wa CSR Barrick North Mara.

DED Solomon Shati

DED Shati anasema utekelezaji wa miradi hiyo umekidhi thamani ya fedha (value for money) na utekelezaji wa miradi mingine unaendelea kwa kasi.

Anasema bajeti ya utekelezaji wa miradi yote kwa sasa inafikia shilingi bilioni 7.3, ambapo shilingi bilioni 6.5 zimeelekezwa kwenye miradi mipya na miradi viporo imechukua shilingi milioni 900.

“Ubora wa kazi ni mzuri na awamu ya pili inaendelea vizuri,” DED Shati anasema.

Wakati huo huo, wazabuni/ wakandarasi wote wakiwemo mafundi waliopata kazi ya kutekeleza miradi hiyo walikuwa wamelipwa fedha zao kufikia wiki iliyopita, isipokuwa mmoja ambaye nyaraka za madai yake zilionekana kuwa na changamoto - ambayo hata hivyo ilikuwa inatafutiwa ufumbuzi.


“Wazabuni/ wakandarasi wote na mafundi wamelipwa fedha zao kwa kazi ya awamu ya kwanza, huyo mmoja naye malipo yake yanashughulikiwa,” DED Shati anaeleza.

Baadhi ya wazabuni na wakandarasi waliozungumza na Sauti ya Mara wanasema utekelezaji wa miradi hiyo umekwenda vizuri kama ilivyopangwa.

“Mimi mwenyewe nimeshalipwa kwa kazi ambazo zilifanyika awamu ya kwanza, na majengo yangu mengi yameshaezekwa, mengine yanaendelea kuezekwa,” anasema Range Boaz, Mkurugenzi wa Ingwe Enterprises Ltd.

Boaz anasema kampuni yake ilipewa kazi ya kujenga vyumba 14 vya madarasa, nyumba tatu za walimu na jengo la utawala, katika shule mbalimbali za msingi na moja ya sekondari - zilizopo jirani na mgodi wa North Mara.

Wataalamu wakikagua mradi uliokamilika

Boaz ambaye ni mmoja wa wazabuni wazawa ambao wameonesha umahiri mkubwa katika kutekeleza miradi hiyo kwa wakati, anasema wapo tayari kupewa miradi mingine ya CSR kutoka mgodi huo, na kuahidi kuendelea kuitekeleza kwa viwango vinavyotakiwa.

“Ushirikiano tunaopata kutoka ofisi ya Mkurugeni Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime pamoja na mgodi wa North Mara ni mzuri, na tupo tayari kupewa miradi mingine ya CSR hata sasa hivi,” anasema Boaz.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Kampuni ya Barrick imekuwa ikitenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya kugharimia miradi ya kijamii kupitia mpango wake wa CSR katika vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi wa North Mara tangu mwaka 2019.

Lakini kwa mara ya kwanza, kipindi hiki viijiji 77 vya halmashauri hiyo vilivyokuwa vinaachwa kando vimepewa asilimia 30 ya ‘keki’ hiyo ya CSR, huku asilimia 70 ikibaki kwenye vijiji 11. Miradi ya kijamii iliyopewa kipaumbele ni elimu, afya na maji.

Utekelezaji wa miradi hiyo unatarajiwa kuboresha huduma za kijmii kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) mkoani Mara.

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages