NEWS

Sunday 30 April 2023

RUWASA kutumia bilioni 7.5 kugharimia utekelezaji miradi ya maji Tarime kwa mwaka 2023/2024



Na Mwandishi Wetu, Tarime
-----------------------------------------

WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Tarime imepanga kutumia shilingi bilioni 7.5 kufanikisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji katika mwaka wa fedha 2023/2024.

Meneja wa RUWASA Tarime, Mhandisi Malando Masheku (pichani juu) alisema hayo katika kikao cha mwaka cha wadau wa maji kilichofanyika mjini hapa juzi kujadili utekelezaji wa miradi ya maji kwa mwaka 2022/23 na mipango ya mwaka 2023/2024.

“Katika mwaka wa fedha wa 2023/2024, RUWASA Wilaya ya Tarime inatarajia kutumia shilingi Bilioni 7.5 katika miradi yake itakayohusisha ujenzi wa matenki ya kuhifadhia maji, uchimbaji visima na ukarabati wa miradi ya zamani,” alisema Mhandisi Masheku na kufafanua kuwa kati ya kiasi hicho cha fedha, milioni 325 zitagharimia urakabati wa miradi ya zamani.

Alitaja miradi mipya ya RUWASA Tarime kwa mwaka 2022/2023 kuwa ni Tagota, Itununu, Kemakorere/ Nyarero, Nyamwigura ambayo utekelezaji wake umefikia asilimia 45 na Regicheri (asilimia 20).


Aidha, Mhandisi Masheku alibainisha kuwa upatikanaji wa maji katika mji wa Tarime kwa sasa ni asilimia 73.3 na kwamba utekelezaji wa miradi ya Mtana, Surubu, Kitawasi na Nyangoto umefikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Mei 30, mwaka huu.

Mwenyekiti wa kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Michael Mntenjele aliwataka wananchi kulinda na kutunza miradi ya maji na miundombinu yake kwa manufaa ya jamii nzima.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages