NEWS

Monday 1 May 2023

Serikali yaipatia Professor Mwera Foundation kibali cha kufanya kazi na mikoa yote Tanzania Bara


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba (kushoto) akimkabidhi Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera cheti cha pongezi na shukrani baada ya taasisi hiyo kutoa tuzo za heshima kwa washindi wakati wa mkutano wa wadau wa elimu mkoani Singida, Alhamisi iliyopita.

NA MWANDISHI WETU, Singida
------------------------------------------------

OFISI ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeipatia Professor Mwera Foundation (PMF) kibali cha kufanya kazi zake na mikoa yote nchini baada ya kufanya vizuri katika mikoa 10 ya awali.

“Baada ya kupewa kibali na Wizara ya TAMISEMI cha kufanya kazi zetu ndani ya mikoa 10, sasa tumeaminiwa zaidi na kupewa kibali na wizara cha kufanya kazi za PMF ndani ya nchi nzima.

“Kibali chetu wamepewa Makatibu Tawala wa Mikoa nchi nzima kuelekezwa watupe ushirikiano tufikapo mikoani mwao,” Mkurugenzi wa PMF, Hezbon Peter Mwera alisema wakati wa mkutano wa wadau wa elimu mkoani Singida, Alhamisi iliyopita.

Katika mkutano huo, PMF nayo ilitunukiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida cheti cha shukrani, ikiwa ni kutambua mchango wa taasisi hiyo kama mdau muhimu wa maendeleo elimu katika mkoa huo.

Hezbon (kulia) akisalimiana na Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Dkt Baganda Elpidius.

Hezbon alisema PMF imejikita zaidi katika kuhamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi wakati wanasubiri matokeo ya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na sita, na hata darasa la saba ili kupata stadi za ufundi zitakazowawezesha kujiajiri, au kuajiriwa na hivyo kuondokana na utegemezi katika familia na jamii kwa ujumla.

Kwa mujibu wa Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa, PMF inatoa mafunzo ya ufundi kwa vijana kupitia chuo chake kijulikanacho kwa jina la Tarime Vocational Training College kilichopo mjini Tarime, Mara na kwamba hadi sasa kina uwezo wa kuhudumia vijana 1,000 kwa wakati mmoja.

Alifafanua kuwa baada ya kupata kibali cha TAMISEMI kwa ajili ya kufanya kazi na mikoa yote Tanzania, PMF imeanza na mkoa wa Singida. “Mikoa mingine itafuata kutegemeana na programu za mkoa husika,” alisema.

Kabla ya hapo, PMF ilikuwa imepewa na Serikali kibali cha kufanya kazi katika mikoa 10; ambayo ni Mara, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu, Kigoma, Katavi, Rukwa na Ruvu.

“Taasisi yetu ni non-profit (isiyotafuta faida) inayojishughulisha na elimu kuanzia shule za msingi, sekondani na vyuo vya mfunzo ya ufundi. Tunahamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi ndani ya mikoa, tunatambua umuhimu wa vijana kupata elimu ya mafunzo ya ufundi.

“Pia inashirikiana na ofisi za wakuu wa mikoa kutoa tuzo na zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya darasa la saba, kidato cha nne na cha sita,” alisema Hezbon.


Hivi karibuni, PMF ilimtunuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan tuzo maalumu ya heshima kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Hezbon alikabidhi tuzo hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kwa ajili ya kuifikisha kwa Rais Samia, wakati wa kikao kazi cha wadau wa elimu wa mkoa huo kilichofanyika mkoani humo.

“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan anajitahidi kufanya mambo mengi ya kuboresha sekta ya elimu nchini, nasi pia kama taasisi, kwa kutambua mchango wake mzuri katika sekta ya elimu, tunamtunuku tuzo maalumu ya heshima, tunaikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma apokee kwa ajili ya kumfikishia Mheshimiwa Rais,” alisema.

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages