NEWS

Thursday 27 April 2023

TAHOSSA wakabidhi matofali 1,000 kuchangia ujenzi wa bweni la wanafunzi Tarime SekondariNa Mara Online News
-----------------------------------

CHAMA cha Wakuu wa Shule za Sekondari Tanzania (TAHOSSA) Wilaya ya Tarime umeipatia Shule ya Sekondari Tarime msaada wa matofali 1,000 kuchangia ujenzi wa bweni la wanafunzi.

Makabidhiano ya matofali hayo yamefanyika shuleni hapo leo katika hafla fupi iliyowashirikisha Mkuu wa Shule, Mwalimu Maro Chenge na Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Lawrent Mwita, miongoni mwa viongozi wengine.

Mwalimu Chenge ameishukuru TAHOSSA kwa mchango huo, akisema shule yake pia imechangia matofali 1,000 yaliyopatikana kutokana na kampeni ya ujenzi wa bweni jipya.

Ujenzi wa bweni jipya unahitajika ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi walioongezeka shuleni hapo kwa mwaka wa Masomo uliopita.

“TAHOSSA wametukabidhi matofali 1,000, pia sisi kama shule tumeunga mkono kwa kuchangia matofali 1,000 kutokana na uwepo wa wanafunzi wengi kwenye mabweni. Sisi kama shule tuliona tuanzishe kampeni ya kujenga bweni jipya ambalo litachukua wanafunzi 120,” ameeleza Mwalimu Chenge.

Katika hatua nyingine, imefanyika ibada maalumu ya kuwaombea wanafunzi wa kidato cha sita shuleni hapo wanaotarajiwa kuanza Mtihani wa Taifa Jumanne ijayo.

Ibada hiyo imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji wa Tarime Simbanilo Changiki ambaye amewahimiza wanafunzi kutojihusisha na vitendo vinavyoweza kusababisha kufutiwa mtihani.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages