NEWS

Tuesday 25 April 2023

TANAPA wakagua miradi ya ujirani mwema Nyanungu na Kwihancha, Mkuu wa Hifadhi Serengeti apongeza kasi ya ujenzi nyumba za walimuNa Waandishi Wetu, Tarime
-------------------------------------------

KAMATI ya Usimamizi wa Miradi kutoka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) imekagua miradi inayotekelezwa chini ya mpango wake wa ujirani mwema katika kata za Nyanungu na Kwihancha zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) mkoani Mara.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Izumbe Msindai ameongoza shughuli hiyo leo Aprili 25, 2023 na kupata fursa ya kuteta na viongozi wa kamati za ujenzi wa miradi hiyo, wakiwemo wenyeviti wa serikali za vijiji katika maeneo ya miradi hiyo.

Miradi hiyo ambayo inagharimu shilingi milioni 287.5 ni pamoja na ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika Shule ya Msingi Kegonga iliyopo katani Nyanungu utakaogharimu shilingi zaidi ya milioni 70.

Mradi mingine ni ujenzi wa nyumba tatu za walimu katika Shule ya Msingi Byantang’ana iliyopo kijiji cha Nyabirongo katani Kwihancha utakaogharimu shilingi milioni 104 na ujenzi wa zahanti katika kijiji cha Karakatonga utakaogharimu shilingi milioni 112.

Msindai ameeleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo, hususan upande wa kata ya Kwihancha.

“Kazi yenu ni nzuri na inaonekana, niwapongeze sana, kama fundi alivyosema mwezi wa sita (Juni) anakabidhi jengo, hongereni sana,” Mkuu huyo wa Hifadhi ya Serengeti amesema wakati wa ukaguzi wa jengo la nyumba za walimu katika Shule ya Msingi Byantang'ana.
Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, Msindai (kushoto) akisalimiana na Diwani wa Kata ya Kwihancha, Ragita.

Kwa upande wake, Afisa Uhifadhi - Ujirani Mwema wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Robert Masobeji amesema ni muhimu wananchi wa maeneo ambayo miradi hiyo inatekelezwa kuchangia asilimia 10 ya gharama ya kila mradi.

“Sisi kama TANAPA tunatoa fedha kulingana na muongozo uliopo, tunatoa asilimia 90 ya gharama za mradi, na asilimia 10 inayobaki ni jukumu la wananchi, viongozi muwaelimishe ili watimize wajibu huo,” amesisitiza Masobeji.

Aidha, viongozi na wakazi wa maeneo hayo wameishukuru TANAPA kwa kufadhili miradi hiyo, hususan wakisema ujenzi wa zahanati utawapunguzia kero mbalimbali ikiwemo ya kutembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.

“Ninatoa pongezi kwa Hifadhi ya Serengeti, mmetukomboa, na kila mtu anaona. Wanakijiji walikuwa wanapata shida sana,” amesema Diwani wa Kata ya Kwihancha, Ragita Ragita.

Mpango wa ujirani mwema wa TANAPA unachangia uboreshaji wa huduma za jamii katika vijiji vilivyo jirani na Hifadhi za Taifa nchini, ikiwemo Serengeti.

Pamoja na mambo mengine, mpango huo unalenga kuwafikia wananchi waishio jirani na Hifadhi za Taifa ili kuwajengea uelewa na kuwafanya kuwa sehemu ya juhudi zinazofanywa na TANAPA katika uhifadhi wa maliasili za wanyamapori na mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages