NEWS

Tuesday, 4 April 2023

Zakayo Wangwe ‘awachana’ Waitara na Tiboche, ataka CCM na vyombo vya dola viwahoji kutokana na vitisho na uchochezi wa kuipinga Serikali uwekaji bikoni mpaka wa Hifadhi ya Serengeti na vijiji viwili katani Nyanungu


Zakayo Chacha Wangwe

Na Mara Online News
------------------------------------

KADA kijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Zakayo Chacha Wangwe amekishauri chama hicho tawala na vyombo vya dola kuwachukulia hatua Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (CCM) na Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard (CCM) kutokana na kauli zao za uchochezi wa kuipinga Serikali huku wakipotosha wananchi juu ya suala la uwekaji wa bikoni za mpaka wa Hifadhi ya Taifa Serengeti na vijiji vinavyopakana nayo upande wa Tarime.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Tarime leo, Zakayo ambaye ni mtoto wa Chacha Zakayo Wangwe aliyewahi kuwa Mbunge wa Tarime, amesema kauli hizo ambazo Waitara na Tiboche walizitoa kwenye mkutano wa hadhara kijijini Kegonga hivi karibuni, ni za kichochezi, ubaguzi wa kikoo na matumizi mabaya ya wazee wa mila ili kuumiza vijana wa kike na kiume katika vijiji hivyo.

“Naomba nitumie nafasi hii kukishauri chama changu cha Mapinduzi kiwaite ndugu zetu hawa Tiboche na Witara wawasikilize, wawahoji na ikionekana wana hatia basi waweze kuonywa, wapewe adhabu hata ya onyo,” amesema Zakayo na kuongeza:

“Nashauri pia vyombo vya ulinzi na usalama viwaite viwahoji na viwafuatilie kwa karibu kwa sababu Mbunge anasimama hadharani anasema ‘kuna watu wanaandika-andika hapa taarifa wanajifanya ma- snitch, sasa tutaanza kuwafuatilia mmoja mmoja, kuwatafuta mmoja mmoja’. Kuwatafutaje? Wanataka kuwafanya nini?”

Zakayo ametumia nafasi hiyo pia kumkosoa Waitara kutokana na kauli zake za vitisho - zenye viashiria vya ubaguzi wa kikoo na zinazotishia amani katika jamii, hususan wananchi wanaoishi kata zinazopakana na Hifadhi ya Serengeti upande wa Tarime.

“Mwita Waitara anafikia kusema ‘hakuna Mwiregi atakayebaki ndani, anawataka Wairegi wote wapigiane simu nchi nzima - walioko Dar es Salaam, walioko Dodoma, walioko Tarime mjini na maeneo mengine wakutane katikati ya Bwiregi ili waweze kusema jambo lao na kwamba wako tayari kwa mapambano, Serikali au Polisi waandae mabomu ya kutosha, waandae na risasi za kutosha’.

“Nguvu hii anayofikiri anaweza kuitumia na anadhani itawasaidia wananchi haiwezi kuwasaidia wananchi na badala yake itawaumiza. Sisi katika hilo hatutakuwa tayari na hata wananchi hao wa Bwiregi anaowahamasisha kwamba wamuunge mkono kwenye haya mambo wengi wao wamesema hawako tayari katika hilo na hawako tayari kuchonganishwa na Serikali.

“Kwa karne hii hatutaki kui- entertain (kukumbatia) masuala ya koo, ubaguzi wa koo, rangi, dini, makabila na kadhalika. Niwaombe wazee wetu wa mila wajitenge na huyu mtu siyo muunganishaji, kwa sababu kijana msomi aliyeelimika vizuri hawezi kutumia wazee kuwashughulikia wananchi wenzake.

“Yaani leo kama ukiwa kijana wa Bwiregi umetofautiana na Waitara mtazamo hata kama ni kumshauri kwamba mheshimiwa mbunge hapa unapotoka, anakwenda kukushtaki kwa wazee wa mila, wazee wa mila watakuita watakushughulikia kweli kweli na kwa sababu wazee wetu tunawaheshimu basi. Mimi niwaombe wazee wale wajiepushe na huyu mtu.

“Namuomba Waitara ajitofautishe na wanaharakati, akiwa na shida zake na malalamiko ya wananchi afuate chaneli (taratibu) za chama, badala ya kuwakilisha wananchi, badala ya kutusemea anaanzisha vurugu anataka kutuhatarishia amani hapa na sisi hatutakuwa tayari kwa hilo,” amesema Zakayo.

Kuhusu kauli ya Tiboche ya kutaka kujiuzulu udiwani, Zakayo amemtaka kuacha kutishia wakubwa ‘nyau’ kuhusu dhamira yake hiyo hiyo.

“Anasema yuko tayari kwa lolote hata kama ni udiwani atajiuzulu. Ukitaka kujiuzulu hutishii, mimi nimekuwa Diwani wa Kata ya Turwa hapa, baada ya kutofautiana na wenzangu wa CHADEMA niliamua kujiuzulu bila kutisha mtu, sikumtisha Mbowe, sikutisha viongozi wangu - niliandika barua. Kwa hiyo ninawashauri Tiboche na Waitara kama wana mpango wa kujiuzulu wajiuzulu salama bila kutisha mtu, bila kuumiza wananchi. Nasikia wana njama za kuhama chama - wahame ni haki yao pia, wakafanyie huko uanaharakati. Chama Cha Mapinduzi siyo chama cha harakati, ni chama cha ukombozi, ni chama chenye heshima,” amesema Zakayo.

Hivi karibuni Tiboche akizungumza katika mkutano wa hadhara kijijini Kegonga alidai kuwa udiwani wake hauna maana na kwamba chama chake kikitaka atauachia. “Ndugu zangu mimi niliwambia, narudi tena kusema leo kwenye mkutano huu, udiwani wangu hauna maana yoyote, kama ni udiwani wauchukue,” alisema.

Aidha, Tiboche aliwashangaza wengi kwa kauli yake ya kutaka wanyamapori wawekewe vituo vya kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

“Mwaka 2024, 2025 waje waweke vituo pale - nyumbu wajiandikishe, tembo wajiandikishe ili wapige kura,” Tiboche alikaririwa akitamka ‘live’ maneno hayo katika mkutano huo.

Kwa sasa Serikali inatekeleza mpango wa kuweka bikoni ili kutatua mgogoro wa muda mrefu wa kugombea mpaka wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na vijiji vinavyopakana nayo upande wa wilaya ya Tarime, vikiwemo Kegonga na Nyandage vya katani Nyanungu.

Uwekaji wa vigingi hivyo ni utekelezaji wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kutokana na ushauri wa Kamati ya Mawaziri Wanane wa Kisekta iliyoundwa na Serikali kukusanya maoni ya ufumbuzi wa migogoro ya ardhi kati ya wananchi na Hifadhi za Taifa nchini, ikiwemo Serengeti.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages