Muonekano wa daraja la mto Tigithe eneo la Nyamongo mapema leo asubuhi
Na Mwandishi wetu, Nyamongo
----------------------------------------------
HALI ya daraja la mto Tigithe eneo la Nyamongo wilayani Tarime imerejea kuwa shwari, na magari yanavuka kama kawaida, TANROADS imesema.
“Barabara sasa hivi inapitika vizuri, hakuna shida yoyote tena, daraja la mto Tigithe lipo sawa na hakuna tatizo,” Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe ameiambia Mara Online News kwa njia ya simu leo.
Timu ya wataalamu kutoka TANROADS imefika eneo hilo mapema leo asubuhi na kujiridhisha kuwa hali ya daraja hilo ni shwari. “Daraja lipo vizuri, magari yanapita bila shida,” amesema Mhandishi Maribe.
Hata hivyo Meneja huyo wa TANROADS ametoa wito kwa wananchi kuchua tahadhari yanapotokea mafuriko katika eneo hilo kama ilivyotokea kwa saa kadhaa jana.
“Cha muhimu wananchi wakiona maji yanakuwa mengi wasipite, wasuburi mpaka yaishe,” ameshauri.
Daraja hilo la mto Tigithe lipo katika barabara kuu ya Serengeti - Tarime na Nyamongo – Tarime, ambayo iko kwenye mpango wa kujengwa na Serikali kwa kiwango cha lami.
Jana jioni, makumi ya magari ya abiria na mizigo yalikwama kuvuka daraja hilo kutokana na mvua iliyonyesha kwa saa kadhaa na kusababisha mafuriko.
Magari yaliyokwama katika eneo hilo ni yaliyokuwa yanatoka Arusha, Serengeti na Nyamongo kwa upande mmoja, na yaliyokuwa yanatoka Tarime kuelekea Nyamongo, Serengeti na Arusha.
#Tunakuhabrisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment