NEWS

Thursday 18 May 2023

Halmashauri Tarime Mji yapata hati safi, Mwenyekiti Komote amshukuru Rais Samia kuing’arisha kwa miradi ya kijamii


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Daniel Komote (aliyesimama) akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani, jana. Waliokaa ni Makamu Mwenyekiti, Thobias Ghati (kulia ) na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Gimbana Ntavyo.

Na Mara Online News
----------------------------------

HALMASHAURI ya Mji wa Tarime mkoani Mara imepata hati safi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo kilichofanyika kwenye ukumbi wao, jana Mei 17, 2023.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniel Komote amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia fedha za kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii na kupunguza kero kwa wananchi.


“Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia, kipindi kilichopita [akimaanisha 2021/2022] tumepata fedha nyingi za miradi ambazo zimetusaidia kupunguza adha ya michango kwa wananchi wetu,” alisema Komote.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, katika kipindi hicho serikali iliipatia halmshauri hiyo shilingi bilioni 1.537 kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya elimu, miongoni mwa mingine.

“Shilingi bilioni 1.537 siyo haba, zimesaidia kujenga matundu 54 ya vyoo 54, vichomea taka viwili kwenye shule za msingi, majengo ya utawala, madarasa ya mfano na ya kawaida 42 na shule za msingi mpya mbili.

“Halmashauri yetu imeendelea kung’aa, kila kata ina miradi, naomba madiwani na wataalamu wa halmashauri yetu tuendeleze ushirikiano,” alisema Komote ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nkende.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages