NEWS

Wednesday 10 May 2023

RC Mzee mgeni rasmi mkutano wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mara keshokutwa


Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee.

Na Mara Online News
------------------------------------

MKUU wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mungiya Mzee anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika mkutano maalumu wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika mkoani humo keshokutwaa Ijumaa.

Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa leo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Maendeleo ya Ushirika Mkoa wa Mara, Momanye Range, mkutno huo utafanyika kwenye ukumbi wa Mwembeni Complex mjini Musoma kuanzia saa 2:00 asubuhi.

Range amesema wanaandaa mkutano huo kwa kushirikiana na Ofisi ya Mrajis Msaidizi wa Mkoa huo, na kwamba utakuwa na mada za elimu na mafunzo mbalimbali kwa wanaushirika, kujadili fursa, masoko na changamoto zinazoikabiri sekta ya ushirika mkoani Mara.

“Katika mkutano huo ambao ni wa kwanza kufanyika mkoani Mara, wanaushirika watapata nafasi ya kuonesha serikali mafanikio na mchango wa ushirika katika maendeleo ya taifa, pamoja na changamoto zinazowakabili,” amefafanua Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya Mkutano huo, Samwel Gisiboye katika mazungumzo na Mara Online News.

Gisiboye ameongeza kuwa idadi ya washiriki wa mkutano huo inatarajiwa kuwa zaidi ya 500 kutoka vyama vyote vya ushirika mkoani Mara na wadau wa ushirika kutoka ndani na nje ya mkoa huo.

Aidha, Gisiboye ambaye pia ni Meneja Mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Mara (WAMACU Ltd), amesema mkutano huo ni sehemu ya maandalizi ya Siku ya Ushirika ambayo huadhimishwa nchini Juni kila mwaka.

Vyama vya ushirika katika mkoa wa Mara vimejikita zaidi katika uzalishaji wa mazao ya kimkakati kama vile pamba, kahawa, tumbaku, masuala ya madini na uvuvi, miongoni mwa mengine.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages