Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Apolinary Lyambiko (kushoto) akikabidhi mfano wa hundi ya msaada wa Dola 10,000 kwa Msimamizi wa Kituo cha Kulea Watoto wenye Ulemavu cha St. Justin, Sista Juliana Kitela leo.
Na Mwandishi Wetu, Musoma
------------------------------------------------
KITUO cha Kulea Watoto wenye Ulemavu cha St. Justin kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara, kimepokea msaada wa Dola za Kimarekni 10,000 (sawa na shilingi za Kitanzania zaidi ya milioni 20), kutoka Kampuni ya Barrick kupitia Mgodi wake wa Dhahabu wa North Mara.
Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi huo, Apolinary Lyambiko amekabidhi msaada huo kwa Msimamizi wa Kituo hicho, Sista Juliana Kitela leo Alhamisi Mei 11, 2023, mbele ya wafanyakazi wengine na watoto wanaopata malezi maalumu kituoni hapo.
Furaha ya kupokea msaada
GM Lyambiko amesema msaada huo umetoka Shirika Lisilo la Kiserikali la NVEP linaloshughulikia changamoto zinazokwamisha maendeleo katika jamii ya Kiafrika, lililoanzishwa na Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Dkt Mark Bristow, mwaka 2010.
“Shirika hili [NVEP] linajikita kutafuta fedha ili kusaidia makundi maalumu katika jamii kama vile wanawake, watoto na mengine yenye uhitaji wa ukuaji wa kiuchumi,” amesema.
GM Lyambiko akizungumza
Lyambiko ameongeza kuwa kila robo ya mwaka NVEP ina utaratibu wa kuelekeza misaada katika masuala yanayolenga kuleta tija na manufaa ya moja kwa moja kwenye jamii zenye uhitaji, na kwamba hadi sasa limeshasaidia mashirika 12 nchini Tanzania.
“Leo tunakabidhi msaada wa Dola 10,000 katika kituo cha watoto wenye mahitaji maalumu cha St. Justin kupitia NVEP. Kituo hiki ni sehemu muhimu ya jamii yetu, kimeonesha kuwathamini watoto hawa kwa jinsi walivyo bila kuwabagua kwa rangi, dini au kabila,” amesema GM Lyambiko.
Picha ya pamoja
Awali, Msimamizi wa Kituo hicho, Sista Juliana ameishukuru Kampuni ya Barrick akisema msaada huo utapunguza changamoto zikiwemo za kitengo cha jiko katika kituo hicho, ili kuimarisha huduma za malezi na kuwajengea watoto hao uwezo wa kujitegemea katika jamii.
Sista Juliana amebainisha kuwa Kituo cha St. Justin kinalea watoto wenye ulemavu wa viungo, akili na viziwi kwa kuwapatia huduma maalumu na muhimu, zikiwemo za chakula, malazi, matibabu, elimu na mafunzo ya useremala na ushonaji.
Sista Juliana akizungumza
Kwa upande wake, Mwanzilishi wa Kituo hicho, Sista Magreth John ameishukuru Kampuni ya Barrick na kuiomba huo usiwe mwisho wa kuwakumbuka kwa misaada zaidi. “Mahitaji ya watoto wetu ni mengi,” amesema.
Sista Magreth akizungumza
Naye Sista Regina John ambaye alihusika kupeleka ombi, amewashukuru GM Lyambiko na Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Francis Uhadi kutokana na ushirikiano mkubwa waliompa wakati akifuatilia upatikanaji wa msaada huo.
Sista Regina akizungumza
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya watoto wenzake wanaolelewa katika Kituo cha St. Justin, Ernest Mwita ambaye ni mlemavu wa akili amesema: “Ninawashukuru wageni wetu [Barrick] kufika na kutusaidia, Mwenyezi Mungu awabariki na kuwazidishia pale mlipotoa.”
GM Lyambiko akivishwa skafu na mmoja wa watoto viziwi wanaounda kikosi cha gwaride la ukakamavu la Kituo cha St. Justin.
Kwa mujibu wa mfanyakazi mwandamizi, Stephano Ariyo, Kituo cha Kulea Watoto wenye Ulemavu cha St. Justin kilianzishwa mwaka 2006 na kinaendeshwa na Shirika la Masista Moyo Safi wa Maria Afrika wa Kanisa Katoliki Jimbo la Musoma.
“Kwa sasa kituo hiki kina wafanyakaazi 25 na kinahudumia watoto 110, ambapo 75 wanaishi kituoni na 35 wanaishi kwa wazazi na walezi wao,” amesema Ariyo.
Watoto wenye ulemavu wakionesha umahiri wa kucheza ngoma wakati wa hafla ya makabidhiano ya msaada huo.
Barrick ni kampuni kubwa inayoongoza duniani kwa shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini. Inaendesha mgodi wa North Mara kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment