NEWS

Wednesday 10 May 2023

Wenyeviti waliotangaza kujiuzulu Nyanungu na Gorong’a watengua maamuzi yao


Sehemu ya wenyeviti wa vitongoji na vijiji katika kata za Nyanungu na Gorong'a waliotengua maamuzi yao ya kujiuzulu leo

Na Mara Online News
---------------------------------

TISHIO la kujiuzulu kwa baadhi ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji katika kata za Nyanungu na Gorong’a wilayani Tarime limetenguliwa, Mara Online News inaripoti.

Habari zilizotufikia kutoka vijiji vya Mangucha katani Nyanungu na Masanga katani Gorong’a zinasema tishio hilo limeyeyuka baada ya viongozi wa CCM Wilaya ya Tarime kukutana na kufanya nao mazungumzo leo.

“Wamesitisha na wamegaili kujiuzulu, wamegundua walikuwa wanapotoshwa bure, na sasa wanaendelea na utumishi mwema,” Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Valentine Maganga amethibitisha katika mazungumzo na Mara Online News, hivi punde.

Hata hivyo wenyeviti hao wamemwomba Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwasaidia ili ulipaji wa fidia ufanyike kwa wananchi ambao miji na mashamba yao ‘vimeangukia’ ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti baada ya serikali kuweka vigingi vipya vya mpaka unaowatenganisha na hifadhi hiyo.

“Sasa hivi hawapingani na maamuzi ya serikali lakini wana maombi kwa Mheshimiwa Rais, kwamba pamoja na bikoni (vigingi) kuwekwa wanaomba Rais awakumbuke kulipwa fidia ili wapate mahali pengine pa kununua ardhi, kwa kuwa walitegemea hayo maeneo kwa kilimo, makazi na malisho ya mifugo,” amesema Maganga.

Katibu huyo amesisitiza kuwa tishio la kujiuzulu kwa wenyeviti hao wa vitongoji na vijiji limefutika baada ya vikao hivyo vya leo vilivyoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho.

Juzi, wenyeviti hao walitangaza kujiuzulu nyadhifa zao - wakipinga vigingi vya mpaka vilivyowekwa na serikali kutengenisha maeneo yao na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

Walitangaza maamuzi hayo siku chache baada ya Mawaziri wenye dhamana za TAMISEMI, Ardhi na Maliasili kufika katika kata ya Nyanungu kukutana na wananchi wa eneo hilo na kuwaelimisha uhalali wa mpaka unaowatenganisha na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weled

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages