NEWS

Wednesday 3 May 2023

Makuruma, mke wa Mwenyekiti CCM Mkoa wawapongeza Mara Online na Sauti ya Mara kwa kufungua milango Mugumu-Serengeti


Na Mwandishi Wetu, Serengeti
---------------------------------------------

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma ameupongeza uongozi wa Mara Online na gazeti la Sauti ya Mara kwa kufungua ofisi katika mji wa Mugumu wilayani humo na kuahidi ushirikiano wa dhati kwa vyombo hivyo vya habari.

Katika hotuba yake ya ufunguzi wa ofisi hizo leo, Makuruma amesema wilaya ya Serengeti inakua kwa kasi, hivyo vyombo vya habari ni muhimu kuwepo ili kuripoti habari za maendeleo.

Mwenyekiti Makuruma (wa pili kushoto) wkati wa kukata utepe kuashiria ufunguzi rasmi wa ofisi hiyo. Wa tatu kulia ni Mkurugenzi na CEO wa Mara Online na Sauti ya Mara, Jacob Mugini.

“Serengeti kwa sasa inakua kwa haraka sana kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Tunakwenda kupata barabara ya lami kutoka Tarime, iko hii inayotokea Makutano inakuja mpaka Natta mpaka Mugumu.

“Lakini pia tunakwenda kupata uwanja wa ndege. Kwa hiyo ni mahali ambapo panakwenda kuwa hurb (kitovu) ya kiuchumi. Kwa hiyo vyombo vya habari ni muhimu sana kuwepo mahali hapa kwa ajili ya kuripoti habari hizi muhimu.

“Nawapongeza Mara Online na Sauti ya Mara kwa kuliona hili na kufungua ofisi hapa [Mugumu], namini kwamba ofisi hii baada ya muda si mrefu itakuwa kubwa na itatusaidia sana kuharakisha maendeleo katika eneo hili la Serengeti na maeneo mengine,” amesema Makuruma.

Furaha ikiendelea wakati wa ufunguzi wa ofisi hiyo

Makuruma ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Busawe kwa tiketi ya chama tawala - CCM, amesema vyombo vya habari vya Mara Online News na gazeti la Sauti ya Mara vimekuwa vikifanya kazi nzuri ya kuhabarisha, kuelimisha na kuburudisha jamii kwa weledi.

“Kwa hiyo mimi niwashukuru na niwaahidi kwamba mimi kama Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti pamoja na viongozi wote wa kiwilaya tutaendelea kushirikiana na ninyi kwa namna ya pekee ili maendeleo yaweze kusonga mbele,” amesisitiza kiongozi huyo.

Naye Getruda Chandi ambaye ni mke wa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chadi, amevipongeza na kuvitabiria vyombo hivyo vya habari ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wa mji wa Mugumu na wilaya ya Serengeti kwa ujumla.

“Vyombo hivi navifahamu vinafanya kazi nzuri na vitapata ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wa Serengeti,” amesema Getruda.

Picha ya pamoja

Awali, Mkurugenzi na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Mara Online na Sauti ya Mara, Jacob Mugini amesema lengo la kufungua ofisi hiyo mjini Mugumu ni kusogeza huduma za vyombo hivyo vya habari karibu na wananchi na wadau wa maendeleo.

"Vyombo vyetu vitaendelea kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu kwa kutoa habari na makala zinazochochea na kuhamasisha maendeleo ya kijamii, kiuchumi, uhifadhi na utalii katika wilaya hii ambayo sehemu yake kubwa ni maeneo ya uhifadhi wa wanyamapori, ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Serengeti,” amesema Mugini ambaye pia ni Mwandishi na Mhariri Mtendaji wa vyombo hivyo vya habari.

Kufunguliwa kwa ofisi ya Mara Online na Sauti ya Mara mjini Mugumu kunafanya idadi ya ofisi za vyombo hivyo vya habari kufikia tatu Kanda ya Ziwa baada ya nyingine kufunguliwa jijini Mwanza hivi karibuni, huku ofisi mama ikiwa mjini Tarime, Mara.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages