NEWS

Friday 5 May 2023

Wanafunzi Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime wawasilisha ripoti zao za mazoezi ya vitendo kutoka kwenye taasisi mbalimbali nchini



Na Mara Online News
------------------------------------

WANAFUNZI 118 wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime - kijulikanacho zaidi kama Tarime Vocational Training College, wamewasilisha ripoti zao za mafunzo ya vitendo waliyopata kwa miezi miwili katika taasisi mbalimbali za serikali na binafsi nchini.

Mawasilisho hayo ambayo yalihusu mambo waliyojifunza, changamoto walizokutana nazo, namna walivyokabiliana nazo na mapendekezo yao ya nini kifanyike ili kuboresha zaidi, yalifanyika mbele ya walimu na wanafunzi wote chuoni hapo jana.
Wanafunzi wakiwasilisha ripoti ya mafunzo ya vitendo

Wanafunzi hao walisema mambo mengi waliyojifunza katika taasisi walizokwenda yamewaongezea ujuzi na uzoefu wa fani wanazosoma.

“Nilipofika Halmashauri ya Mji wa Bunda nimejifunza mambo mengi, nimejifunza kuchapa nyaraka za ofisi na jinsi ya kupanga mafaili ndani ya ofisi,” alisema mwanachuo Tulizo Kateba.

Baada ya mawasilisho hayo, Meneja Uendeshaji wa Taasisi ya Professor Mwera (PMF) inayomiliki chuo hicho aliwashauri wanafunzi hao kuendelea kuwa na ujasiri wa kukabiliana na changamoto wanazokutana nazo katika harakati za masomo ili kufikia ndoto zao za kielimu.

“Lakini tunawapongeza kwa sababu wengi wenu mmegundua kwamba baadhi ya changamoto mlizokumbana nazo katika kazi ni sehemu ya fursa ya nafasi nzuri zaidi ya kuendelea kujifunza,” alisema Mwalimu Mwita.
Mwalimu Mwita akizungumza katika hafla hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya PMF, Hezbon Peter Mwera aliwapongeza wanafunzi hao na kuahidi kufanyia kazi na kufikisha kwa taasisi husika mapendekezo waliyotoa kuhusu nini kifanyike ili kuboresha zaidi mazingira ya mafunzo ya vitendo.

“Tumefanya hivi ili pia na vyuo vingine vijifunze kuwa na utaratibu wa kupokea mawasilisho ya ripoti za wanafunzi wanaotoka kwenye mafunzo ya vitendo,” alisema Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa.
Mkurugezi wa Taasisi ya PMF, Hezbon Peter Mwera akiwa ofisini kwake.

Fani zinazofundishwa katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kilichopo mjini Tarime mkoani Mara ni pamoja na ufundi magari, uchomeleaji, udereva, ICT, kompyuta, ukatibu muhtasi, usimamizi wa hoteli na utalii, usaidizi katika maabara na uendeshaji biashara.

Hivi karibuni, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iliipatia Taasisi ya PMF kibali cha kufanya kazi zake na mikoa yote nchini baada ya kufanya vizuri katika mikoa 10 ya awali.

“Baada ya kupewa kibali na Wizara ya TAMISEMI cha kufanya kazi zetu ndani ya mikoa 10, sasa tumeaminiwa zaidi na kupewa kibali na wizara cha kufanya kazi za PMF ndani ya nchi nzima.

“Kibali chetu wamepewa Makatibu Tawala wa Mikoa nchi nzima kuelekezwa watupe ushirikiano tufikapo mikoani mwao,” alisema Hezbon.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages