NEWS

Monday 22 May 2023

Mbunge Chege ashusha msaada wa madawati 360 kwenye shule 20 Rorya, DC, DED, madiwani wampongeza



Na Joseph Maunya, Rorya
-----------------------------------------

MBUNGE wa Rorya mkoani Mara, Jafari Chege amezipatia shule 20 zikiwemo za msingi 19 na moja ya sekondari za jimboni humo msaada wa madawati 360 yenye thamani ya shilingi milioni 20.

Madawati hayo yalipokewa na Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Juma Chikoka katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Nyanduga jana Jumatatu.

Sehemu ya msaada wa madawati uliotolewa na Mbunge Chege

Viongozi wengine waliohudhuria hafla hiyo ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya (DED), Francis Namaumbo na madiwani, miongoni mwa wengine.

Katika hotuba yake, DC Chikoka alimpongeza Mbunge Chege, akisema madawati hayo yatazipunguzia shule husika changamoto, huku akitoa wito kwa wadau wengine kujitokeza kuchangia uboreshaji wa elimu na huduma nyingine za kijamii wilayani Rorya.

“Kiukweli mimi naendelea kumpongeza sana Mbunge [Chege] na namshukuru sana… tutaendelea kufuatilia kwa wadau wengine ili na wao wawe sehemu ya michango na kutatua changamoto za madawati na maeneo mengine,” alisema DC Chikoka.

DC Chikoka akizungumza katika hafla hiyo

Aidha, DC Chikoka alidokeza kuwa wana mpango wa kuanzisha kampeni maalumu itakayogusa wana-Rorya wote ili kuchangia madawati kwenye shule za wilaya hiyo kukabiliana na upungufu uliopo.

“Mwaka huu kabla haujaisha lazima tuje na kampeni maalumu na mahususi ya kuondoa changamoto ya madawati katika shule zetu za msingi na sekondari, hiki kilichofanyika basi na sisi kama serikali tutaongeza thamani pale ambapo Mbunge amefanya,” alisema.

Naye DED Namaumbo alimpongeza Mbunge Chege kutokana na jitihada zake za kubaini changamoto za kimaendeleo katika halmashauri hiyo na kushiriki kuzitafutia ufumbuzi.

DC Chikoka (wa pili kulia), DED Namaumbo (kulia) na viongozi wengine wakionesha mojawapo wa madawati yaliyotolewa na Mbunge Chege.

Kwa upande wao, madiwani wa kata mbalimbali waliohudhuria hafla ya makabidhiano ya msaada huo wa madawati walisema umewapunguzia wazazi mzigo wa kuchangia maendeleo ya shule hizo.

“Sisi tumefurahi sana, Mbunge ametusaidia, kila mdau wa elimu aliyeko ndani na nje ya wilaya hii aige huu mfano kwa sababu mapambano dhidi ya ujinga ni makubwa,” alisema Samson Kagutu, Diwani wa Kata ya Nyahongo.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages