Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
Na Mara Online News
---------------------------------
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa Majaji sita wa Mahakama ya Rufani.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu leo Mei 18, 2023 imewataja waliopata uteuzi huo kuwa ni Jaji Zainab Goronya Muruke aliyekuwa Jaji Mfawidhi, Kituo Jumuishi cha Mashauri ya Ndoa, Talaka na Mirathi - Temeke, Dar es Salaam.
Wengine ni Jaji Dkt Benhajj Shaaban Masoud, ambaye kabla ya kuteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani alikuwa Mkuu wa Shule ya Sheria Tanzania.
Jaji Amour Said Khamis aliyekuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, na Jaji Leila Edith Mgonya ambaye hadi anateuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Masijala Kuu Dar es Salaam.
Wengine walioteuliwa na Rais Samia kuwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ni Jaji Gerson John Mdemu aliyekuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, na Jaji Agnes Zephania Mgeyekwa ambaye kabla ya uteuzi huo alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi.
“Uteuzi huo wa Majaji wa Mahakama ya Rufani umeanza tarehe 28 Aprili, 2023 na wataapishwa tarehe itakayopangwa baadae,” imehitimisha taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment