
Na Christopher Gamaina
Tarime
-------------


Tarime
-------------
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals, leo Juni 5, 2026 umeungana na jamii inayouzunguka kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani, kwa kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi wa kurejesha uoto wa asili wa Mto Tighite.
Tukio hilo limewashirikisha viongozi wa serikali na jamii ngazi ya kata, vijiji jirani na wananchi wa kawaida, ambao wamejionea maendeleo ya ukuaji miti ya asili iliyopandwa kandokando ya mto huo katika kijiji cha Matongo, kupitia Jumuiya ya Watumia Maji Tighite Chini (JWMTC).
Wadau hao wameeleza kuridhishwa na ukuaji wa miti hiyo pamoja na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha mazingira ya mto huo yanarejea katika hali yake ya asili baada ya kuathiriwa na ukataji wa miti ovyo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Meneja Mazingira wa Mgodi wa Barrick North Mara, Frank Ngoloma, amesifu usimamizi na ulinzi mzuri unaofanywa na JWMTC kuhakikisha mradi huo haukwami. “Tumeona miti inaendelea kukua vizuri,” amesema.
Kwa upande wao, Mwenyekiti wa JWMTC, Mwita Seri na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Charles Ryoba, wameushukuru mgodi huo kwa ufadhili na ushirikiano unaoendelea kutoa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Pia, wamesisitiza umuhimu wa kuendelea kuuwezesha mradi huo kifedha na kitaalamu ili kuhakikisha mafanikio yaliyoanza kuonekana yanaendelea kudumu na kuleta matokeo chanya ya muda mrefu kwa mazingira na jamii.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa wananchi kutoka vijiji mbalimbali wameshauri mgodi huo kuangalia pia uwezekano wa kufadhili utekelezaji wa mradi wa aina hiyo katika kingo za Mto Mara.
“Tunaomba mgodi usaidie pia uhifadhi wa mazingira katika Mto Mara kwa sababu kule napo kuna mmomonyoko wa udongo kwenye kingo zake,” amesema Suzana Wilson kutoka kijiji jirani cha Nyabichune.

Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa, JWMTC iliomba Mgodi wa Barrick North Mara ukakubali kutoa shilingi milioni 36.7 kwa ajili ya kuotesha miche kwenye vitalu, kisha kupanda miti ya asili 50,000 katika eneo lenye ukubwa wa hekta 27 kandokando ya Mto Tighite.
Mradi wa kurejesha uoto wa asili wa Mto Tighite unatajwa kuwa na umuhimu mkubwa wa kimazingira kutokana na nafasi ya chanzo hicho cha maji katika mfumo wa ikolojia ya eneo hilo.
Mradi huo ulizinduliwa wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka jana kwa lengo la kurejesha uoto wa asili wa mto huo unaotegemewa na maelfu ya wananchi kwa ajili ya maji ya matumizi ya nyumbani, kunywesha mifugo na shughuli za kilimo.
Aidha, Mto Tighite ni miongoni mwa vyanzo muhimu vinavyochangia maji katika Mto Mara ambao unamwaga maji yake katika la ziwa la kimataifa - Ziwa Victoria upande wa Tanzania.

No comments:
Post a Comment