Na Mwandishi Wetu, Serengeti
-----------------------------------------------
WADAU wa maji wilayani Serengeti, Mara wamekutana kupata taarifa na kujadili utekelezaji wa miradi ya maji na changamoto zake, katika mkutano maalumu ulioandaliwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Mkutano huo ulifanyika katika hoteli ya Giraffe mjini Mugumu jana Jumatatu, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya (DC) hiyo, Dkt Vincent Mashinji.
Taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maji iliwasilishwa na Meneja wa RUWASA Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Deus Mchele.
Mhandisi Mchele akizungumza mkutanoni |
Akifungua mkutano huo, DC Mashinji alisisitiza wajibu wa kila mwananchi kushiriki katika ulinzi na utunzaji wa vyanzo vya maji na mazingira kwa ujumla.
“Ni wajibu wa kila mtu wilayani Serengeti kuchukua hatua zitakazochangia kukomesha vitendo vinavyoashiria uharibifu wa vyanzo vya maji na mazingira,” alisema.
Aidha, DC Mashinji aliihimiza RUWASA kuhakikisha miradi ya maji inaendelea kutekelezwa kwa ufanisi ili kuboresha huduma ya maji kwa wana-Serengeti.
Alitumia nafasi hiyo pia kuzitaka serikali za vijiji vinavyozunguka bwawa la Manchira linalosambaza maji ya bomba kwa wakazi wa mji wa Mugumu na vijiji jirani kuhakikisha haliathiriwi na shughuli za kibinadamu.
DC Mashinji akifungua mkutano huo |
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Serengeti, Mrobanda Japan alisema uboreshaji wa huduma ya maji kwa wananchi ni sehemu ya utekelezji wa Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho tawala.
“Miradi ya maji ikitekelezwa kwa wakati na kwa weledi itakisaidia Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuaminika kwa wananchi na kitaendelea kushika dola kwa kuwa kinasema na kutenda,” alisema Mrobanda.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment