Na Joseph Maunya, Tarime
----------------------------------------
USHIRIKIANO wa madiwani na watumishi umetajwa kuchangia Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini) kupata hati safi kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika mwaka wa fedha 2021/2022.
Hayo yalielezwa na Mkurugenzi Mtendaji (DED), Solomon Shati wakati wa kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo cha kujadili taarifa mbalimbali za kata na vijiji katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2022/2023 kilichofanyika Nyamwaga, jana Mei 12, 2023.
“Nipende kuwajulisha waheshimiwa madiwani kuwa halmashauri yetu imepata hati safi kwa mwaka 2021/2022 katika ripoti ya CAG, hii hati imetokana na ushirikiano wetu katika kutekeleza shughuli za maendeleo ndani ya halmashauri yetu,” alisema DED Shati.
Katika hatua nyingine, DED Shati alisema fedha zilizotolewa na Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR) kwa mwaka wa 2022/23, ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya halmashauri hiyo ni shilingi bilioni 7.3.
DED Shati akizungumza kikaoni. Aliyekaa ni Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Petro Ntogoro Kurate.
“Fedha za CSR ni shilingi bilioni 7.3 ambazo zinaendelea kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kijamii, na tayari kiasi cha shilingi bilioni 3.2 kimekwishatumika na kazi inaendelea. Malipo yote ya mpango wa CSR yanalipwa kutoka mgodini, fedha haziletwi halmashauri.
“Mtakumbuka huko nyuma fedha za CSR zilikuwa zinaelekezwa kwenye vijiji 11 katika kata tano pekee, lakini maboresho yaliyofanyika ni kwamba CSR iliyofuata ambayo ndiyo hii tunayotekeleza, fedha zimekwenda kwenye vijiji na kata zote za halmashauri yetu,” alisema DED Shati.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, halmashauri hiyo ilipanga kukusanya shilingi zaidi ya bilioni 7.935 kwa kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 lakini ikakusanya shilingi zaidi ya bilioni 7.151 sawa na asilimia 90, na kwamba hadi Aprili 2023 ilikuwa imevuka lengo kwa kukusanya shilingi zaidi ya bilioni 7.994 sawa na asilimia 101.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mwema, Petro Ntogoro Kurate aliongeza kuwa hati safi iliyotolewa na CAG imechangiwa pia na usimamizi mzuri wa fedha zinazotolewa na Serikali Kuu pamoja na za CSR Barrick North Mara.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment