NEWS

Tuesday 30 May 2023

Wadau wawataka Watanzania kutodanganyika kuhusu unywaji wa kahawa



Na Mara Online News
--------------------------------

WATANZANIA wametakiwa kutokubali upotoshaji kwamba unywaji wa kahawa unasababisha ugonjwa wa Shinikizo la Damu (Presha).

Badala yake wametakiwa kuchangamkia matumizi ya kinywaji hicho ili kukuza soko la ndani na kuinua uzalishaji wa zao hilo na tija kwa wakulima nchini.

Hayo yameelezwa katika mkutano wa wadau wa zao la kahawa Kanda ya Mara, ulioandaliwa na Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) na kufanyika mjini Tarime, leo Jumanne Mei 30, 2023.
Mkuu wa Wilaya, Kanali Michael Mntenjele (katikati) akimkabidhi Mwenyekiti wa Bodi ya WAMACU Ltd, David Hechei kifaa cha kupima unyevu wa kahawa kilichotolewa na TCB. Kulia ni Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TCB, Edmond Zani.

Hoja ya kupinga upotoshaji kuwa unywaji wa kahawa unasababisha Presha iliibuliwa katika mkutano huo na Mwakilishi wa Chama cha Msingi cha Ushirika na Masoko (AMCOS) Mirare wilayani Rorya, Emmanuel Ndege Benson, akihoji utafiti unaoweza kuthibitisha hilo.

“Baadhi ya watu hawanywi kahawa baada ya kusikia upotoshaji kwamba inasababisha Presha. Ni utafiti gani unaoweza kuthibitisha hilo? Watu waache upotoshaji, wawaache Watanzania wanywe kahawa soko lake liongezeke nchini, tunajua pia kahawa ina mchango kwenye afya ya mwili wa binadamu,” amesema Ndege.

Akichangia hoja hiyo, Meneja wa Taasisi ya Utafiti wa Kahawa Tanzania (TaCRI) Kanda ya Mara, Almas Mshihiri amesema kahawa haina madhara kwa afya ya binadamu, na akatoa wito kwa wananchi kupata elimu sahihi kuhusu matumizi ya kahawa kupitia kwa wataalamu wa kilimo na afya.

“Mimi nawambia kwamba kahawa haina shida ila kila kitu kina matumizi yake inavyotakiwa, kwamba ni gramu ngapi katika mili ngapi za maji uweke kahawa ili unywe kiafya. Kwa hiyo kahawa haina tatizo, kahawa ni nzuri sana kiafya,” amesisitiza Mshihiri.
Mshihiri akiwasilisha mada mkutanoni

Hivyo miongoni mwa maazimio ya mkutano huo wa wadau wa kahawa Kanda ya Mara ni kuongeza juhudi za kuhamasisha Watanzania kuchangamkia unywaji wa kahawa ili kujenga afya, lakini pia kustawisha soko la ndani na kuinua uzalishaji wa zao hilo na tija kwa wakulima nchini.

Mkutano huo wa siku moja umefunguliwa na kufungwa na Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, ambapo mbali na TaCRI, wadau wengine waliohudhuria ni kutoka Chama Kikuu cha Ushirika cha Mkoa wa Mara (WAMACU Ltd).

Wengine ni kutoka JKT Ng’ereng’ere, Kitenga Sisters, NHCCL, Mwitongo Farm, AMCOS, Wakala wa Huduma za Misitu (TFS), NMB, Halmashauri za Tarime na ofisi za Mrajis na Mkuu wa Mkoa.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages