NEWS

Thursday 22 June 2023

RC Mara aitaka Tarime Mji kukamilisha uuzaji viwanja, kulipa deni la wizara

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda akihutubia Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime. Aliyekaa ni Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Daniel Komote.

 

Na Mwandishi wa
Mara Online News
------------------------------

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda ameliagiza Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Tarime kusimamia ukamilishaji wa uuzaji wa viwanja vyenye thamani ya shilingi 464.

RC Mtanda alisisitiza katika kikao cha baraza hilo mjini Tarime jana kwamba uuzaji wa viwanja hivyo uzingatie sheria, kanuni na miongozo ya ununuzi kulingana na maelekezo ya Kamati ya Bunge.

Aidha, aliitaka menejimeti ya halmashauri hiyo kuwasilisha kwenye baraza hilo mpango wa ulipaji wa mkopo wa shilingi milioni 560 uliotolewa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

“Mlipewa mkopo lazima mrejeshe. Kwa hiyo nalielekeza baraza kutengeneza mpango mkakati wa kulipa na namna ya kuviuza hivyo viwanja, na hii nitatoa time frame (muda) hadi tarehe 15 mwezi wa saba, jambo hili liwe limetekelezwa,” alisema.




RC Mtanda alitumia nafasi hiyo pia kuipongeza halmashuari hiyo kwa kupata hati safi katika mwaka wa fedha 2021/2022, lakini pia kwa kutekeleza mradi mkakati wa soko la kisasa la mji wa Tarime, chini ya usimamizi thabiti wa Mwenyekiti wa Halmashauri, Daniel Komote na Mkurugenzi Gimbana Ntavyo.

Hata hivyo, kiongozi huyo wa mkoa aliitaka halmashauri hiyo kuhakikisha inafanya upembuzi yakinifu wa miradi ya maendeleo kabla ya utekelezaji wake, ili kuepuka hoja za ukaguzi.

“Kwa hiyo tusiibue miradi kisiasa, ni kukiuka sera,” alisema RC Mtanda na kuhitimisha hotuba yake kwa kuitaka halmashauri hiyo kurekebisha maeneo yenye mapungufu, ili iendelee kupata hati safi.


#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages