NEWS

Tuesday 13 June 2023

Rais Samia ateua viongozi mbalimbali, Katibu Mkuu Kiongozi awa Balozi

Rais Samia Suluhu Hassan

Na Mwandishi Wetu
---------------------------------

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, akiwemo Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt Moses Mpogole Kusiluka ambaye ameteuliwa kuwa na hadhi ya Balozi.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais - Ikulu, Zuhura Yunus leo Juni 13, 2023 imewataja viongozi wengine walioteuliwa kuwa na hadhi ya Balozi kuwa ni:

Msaidizi wa Rais anayeshughulikia masuala ya Siasa, Dkt Salim Othman Hamad na Msaidizi wa Rais anayeshughulikia masuala ya Hotuba, Dkt Kassim Mohamed Khamis.

Hata hivyo viongozi hao wanaendelea kutumikia vyeo walivyonavyo kwa sasa, kwa mujibu wa taarifa hiyo, na kwamba wataapishwa Juni 16, 2023 kuanzia saa 4:00 asubuhi Ikulu - Chamwino jijini Dodoma.

Wakati huo huo, Rais Samia amefanya uteuzi mwingine ikiwa ni pamoja na kumteua aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Rogatus Hussein Mativila kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais - TAMISEMI (Miundombinu).

Rais pia amemteua Mkurugenzi wa Ufundi wa Wakala wa Usimamizi wa Usalama wa Usafiri wa Anga wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (CASSOA), Mhandisi Mohamed Besta kuwa Mtendaji Mkuu wa TANROADS.

Mwingine ni Kamishna Benedict Wakulyamba aliyeteuliwa na Rais Samia kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, ambapo anachukua nafasi ya Anderson Mutatembwa ambaye amehamishwa kwenda kuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu).

Naye Mhandisi Amin Nathaniel Mcharo ameteuliwa na Rais Samia kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TANROADS.

“Uteuzi huu umeanza tarehe 12 Juni, 2023,” imesema taarifa hiyo ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages