NEWS

Monday 12 June 2023

Wananchi wataja faida za German Road inayoboreshwa na Barrick North Mara



Na Mwandishi Maalumu
----------------------------------

UKARABATI wa barabara ya German (German Road) ulioanza miezi michache iliyopita kwa gharama za Kampuni ya Barrick kupitia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, umewajaza matumaini makubwa wakazi wa vijiji husika wilayani Tarime.

Barabara hiyo ya kiwango cha changarawe - yenye urefu wa kilomita 45 imekuwa haipitiki kirahisi kwa miaka mingi, na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa watumiaji, wakiwemo wakazi wa vijiji inakopita.

Lakini hatimaye imeanza kufanyiwa maboresho makubwa kwa gharama za mgodi wa North Mara unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Viongozi na wakazi wa vijiji inakopita barabara hiyo wameeleza kupokea kwa furaha hatua hiyo ya kuikarabati, wakisema itawafungulia ukurasa mpya wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Endapo ukarabati wa barabara hii utakamilika utakuwa imetuondolea kero ya miaka mingi ya kutopitika kwa urahisi na hivyo kutukwamisha kimaendeleo,” anasema mkazi wa kijiji cha Nyakunguru, Matiko Nyaiho katika mazungumzo na Sauti ya Mara kijijini hapo, wiki iliyopita.

Nyaiho anasema ukarabati huo pamoja na mambo mengine, pia utawaondolea kero ya kutopitika kirahisi kwa daraja la mto Gokohe - maarufu kwa jina la Daraja Mbili wakati wa misimu ya mvua.

“Tunaona madaraja yanajengwa kwa uimara wa kudumu, hata kwenye daraja hili watatuondolea shida ya kuvuka ambayo tumekuwa tukipata wakati wa mvua,” anasema Nyaiho ambaye pia ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime kutokea Tawi la Nyakunguru.

Faida nyingine zitakazotokana na ukarabati wa German Road ni pamoja na kuwezesha wanafunzi kuhudhuria masomo kikamilifu bila kikwazo cha kuharibika kwa miundombinu ya barabara.

“Kuna Shule ya Sekondari Genge wanafunzi wake wanavuka mto Gokohe kutoka Nyarwana kuja huku Nyakunguru, lakini pia kuna Shule ya Sekondari Kibasuka watoto wanatoka Nyakunguru wanavuka mto huo wanakwenda kusoma huko. Mvua ikinyesha huwa watu hawavuki, na wanafunzi hawaendi shule kabisa.

“Kwa hiyo uboreshaji wa barabara hii na madaraja yake utakuwa umetuondolea kero ya kubwa na wanafunzi watapata faida kubwa maana watapata elimu kwa manufaa ya taifa letu,” anasema kada huyo wa chama tawala - CCM.

Anaongeza kuwa ukarabati wa barabara hiyo utawarahisishia wakazi wa vijiji husika kuanzia Nyamongo, Nyakunguru, Nyarwana hadi Komaswa usafiri wa kwenda miji ya Tarime, Musoma na Mwanza. “Hii barabara ya German hata kwa watu wanaokwenda Tarime mjini ni karibu zaidi ukipitia Mtana kuliko kuzunguka Nyamwaga” anasema.

Wanavijiji wanataja faida nyingine kuwa ni kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo kwenda kwenye masoko, minada na miji inakopita barabara hiyo ya German.

Achilia mbali kwamba barabara hiyo pia inatumiwa na magari makubwa ya mgodi wa North Mara kufuata na kuingiza bidhaa mbalimbali kama vile mafuta na mitambo kwa ajili ya shughuli za uchimbaji madini.
Sehemu ya German Road ambayo ukarabati umekamilika katika kata ya Kibasuka

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Nyakunguru, Chacha Makuri anaamini kwamba ukarabati huo utawezesha kushuka kwa nauli za usafiri wa magari na pikipiki (bodaboda) - ambazo anasema zimekuwa zikipanda kutokana na ubovu wa barabara hiyo.

Naye Awino Chacha Kabasi ambaye ni Katibu wa Umoja wa Wanawke Tanzania (UWT) wa CCM Tawi la Keisaka inakopita barabara hiyo anasema ukarabati huo ni faraja kwa wakazi wa kijiji cha Keisaka kipindi hiki wanachoelekea kujenga soko la kimkakati kijijini hapo.

“Tuna mpango wa kujenga soko kubwa katika kijiji chetu, hivyo tunatarajia kuneemeka na ukarabati wa German Road maana wafanyabiashara watapata urahisi wa kusafiri kutoka maeneo tofauti kuleta bidhaa mbalimbali kwenye soko hilo,” anasema Awino.

Awino ambaye pia ni Mjumbe wa Serikali ya Kijiji cha Keisaka ambacho ni miongoni mwa vijiji ambako ukarabati wa barabara hiyo umekamilika, anaishukuru Kampuni ya Barrick, akisema maeneo yaliyokuwa yameharibika na kusababisha wanafunzi kupita kwa shida kwenda shule na kurudi nyumbani yamerekebishwa.

“Kabla ya ukarabati wa maeneo haya watoto wetu wamekuwa wakishindwa kwenda shule maana njia ilikuwa imeharibika sana, hata magari yalikuwa yanakwama, lakini sasa hivi matatizo hayo yamekwisha, tunafurahi sana,” anasema kiongozi huyo.

Anaongeza kuwa ukarabati wa barabara hiyo umewarahisishia pia usafiri wa kwenda kutafuta huduma muhimu za kijamii ikiwemo matibabu kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali.

Kwa ujumla uboreshaji wa barabara hiyo unatarajiwa kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika jimbo la Tarime Vijijini lenye utajiri mkubwa wa madini.

Utarahisisha huduma za usafiri wa magari ya abiria na mizigo kwa wananchi wanaoishi kata tano [Komoswa, Manga, Kiore, Kibasuka na Kemambo] na mgodi wa North Mara kwa upande mwingine.

Maboresho ya barabara hiyo yalibuniwa na mgodi huo ili kuwaondolea watumiaji usumbufu wa kupita na vyombo vya usafiri.

Barabara hiyo inakarabatiwa kwa kiwango cha changarawe kinachohusisha uwekaji wa makaravati ya madaraja, alama za barabarani na barabara za mchepuko.

Taarifa zilizopo sinasema utekelezaji wa mradi huo umegawanywa katika vipande vitatu; cha kwanza chenye urefu wa kilomita 15 kikianzia eneo la Gachuma hadi Kembwi, cha pili Nkerege hadi Nyarwana (km 15) na cha tatu Nyarwana hadi Uwanja wa Ndege chenye urefu wa kilomita 15 pia.

Matumaini ya wanavijiji ni kwamba mgodi huo utaharakisha ukarabati huo, na utakuwa na utaratibu wa kukarabati barabara hiyo mara kwa mara, na au kuijenga kwa kiwango cha lami ili isiharibike tena.

Chanzo: SAUTI YA Mara
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages