NEWS

Monday 5 June 2023

Siku ya Mazingira Duniani 2023: Barrick North Mara washirikiana na jamii kupanda miti



Na Mwandishi Wetu
Mara Online News
-----------------------------

KAMPUNI ya Barrick kupitia Mgodi wa Dhahabu wa North Mara imeshirikiana na jamii inayozunguka mgodi huo kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani leo Juni 5, 2023 kwa kupanda miti.

Katika maadhimisho hayo, mgodi wa Barrick North Mara umetoa msaada wa miche ya miti ya matunda na kivuli ipatayo 200 na kushirikiana na jamii kuipanda katika Shule ya Sekondari ya Matongo wilayani Tarime.


Akizungumza wakati wa upandaji wa miti hiyo, Meneja Mazingira wa mgodi huo, Frank Ngoloma amesema wameelekeza shughuli hiyo katika shule hiyo mpya ili kuiboreshea uoto wa asili na mazingira kwa ujumla.

“Hii shule ni mpya ina uhitaji ya miti kwa ajili ya kukuza uoto wa asili wa eneo hili,” amesema Ngoloma na kuongeza:

“Tumeamua kushirikiana na jamii kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kupanda miti, tumeanzia ndani ya mgodi ambapo wafanyakazi wa kila idara wameshirikiana na viongozi wao kupanda miti, na hii inaonesha commitment (uwajibikaji) ya mgodi katika kulinda mazingira.”
Meneja Frank Ngoloma akipanda mti
Baadhi ya wafanyakazi wa mgodi wa Barrick North Mara wameshiriki kupanda miti ndani ya mgodi huo.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kata (WEO) ya Matongo, Lackson Isibhu ameupongeza mgodi wa Barrick North Mara kwa kuthamini maadhimisho hayo na kuona umuhimu wa kushirikiana na jamii kupanda miti ili kulinda mazingira.

“Tunaushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa kutambua sikukuu za kitaifa na kimataifa. Kati ya taasisi au mashirika yaliyopo katika wilaya yetu ni Barrick North Mara pekee ndio wanafanya tukio kama hili la siku ya mazingira na wanakuja kusaidiana na jamii kuboresha mazingira,” amesema Lackson.
Meneja Ngoloma (wa pili kushoto) katika picha ya pamoja na wafanyakazi wenzake wa Idara ya Mazingira ya mgodi wa Barrick North Mara.

Lackson ametumia nafasi hiyo pia kuwahimiza walimu kusimamia utunzaji wa miti iliyopandwa shuleni hapo, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila mwanafunzi anakuwa na mtu wa kuutunza ili yote ikue vema na kustawisha mazingira ya eneo hilo.

“Tunategemea baada ya miaka kadhaa tutakuwa na miti mingi ya matunda na kivuli, lakini pia hewa safi katika shule hii,” amesema WEO huyo.
WEO Lackson Isibhu kimwagilia maji mti alioupanda

Naye Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Daudi Itembe amesema hatua ya mgodi ya Barrick North Mara kushirikiana na jamii inayouzunguka kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani kwa kupanda miti inadhihirisha uhusiano mzuri uliopo baina ya pande hizo mbili.

“Hili ni jambo la kujivunia na linaonesha kwamba tuna mahusiano ya karibu sana na mgodi huu wa Barrick North Mara,” amesema Itembe.

Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Matongo, Mwalimu Zabron Orege ameushukuru mgodi huo na kuuomba kuangalia uwezekano wa kuisaidia miche ya miti zaidi, miongoni mwa changamoto nyingine zinazoikabili.

“Hii shule ni mpya ilianza mwaka 2021, hivyo bado ina uhitaji mkubwa,” amesema Mwalimu Orege.
Mwalimu Orege akipanda mti shuleni hapo

Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani mwaka huu inasema: “Epuka Uchafunzi wa Mazingira Unaotokana na Mifuko ya Plastiki”.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages