NEWS

Friday 2 June 2023

Ongezeko la watalii limevunja rekodi ya mapato TANAPA - Waziri Mchengerwa



Na Brigitha Kimario, Dodoma
---------------------------------------------

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amesema idadi ya watalii imeongezeka nchini na kumevunja rekodi ya mapato katika Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Waziri Mchengerwa ameyasema hayo wakati akiwasilisha Bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii katika Bunge la 12, mkutano wa 11 kikao cha 39 jijini Dodoma, leo Ijumaa Juni 2, 2023.

“Taasisi za utalii nchini zimevunja rekodi ya mapato katika maeneo yao. Mfano, TANAPA kwa mwaka mzima wa 2021/22 walikusanya TZS bilioni 174, kwa miezi 10 tu ya mwaka huu wa fedha, wameshakusanya TZS bilioni 291. Mapato haya kwa taasisi ni makubwa kuliko yoyote yaliyowahi kukusanywa tangu zianzishwe,” amesema Waziri Mchengerwa.

Aidha, Waziri Mchengerwa amesema mapato hayo yametokana na juhudi zilizofanyika za pamoja kutangaza vivutio vya utalii na kuimarika kwa miundombinu ya utalii ndani ya hifadhi.

Ameongeza kuwa Shirika la TANAPA litaendelea na juhudi zote kuimarisha shughuli zake za ulinzi, ikolojia, kutangaza utalii, kukusanya maduhuli na kuimarisha miundombinu ili kuendelea kuvunja rekodi na watalii kufurika zaidi katika hifadhi zetu.
Waziri Mchengerwa akiwasilisha hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii bungeni

“Shirika litaendelea kuboresha miundombinu ya huduma za utalii kwa kujenga barabara mpya zenye urefu wa kilomita 500 na kukarabati kilomita 10,500. Vilevile shirika litakarabati kilomita 300 za njia ya miguu za kupanda milimani; kujenga mifumo ya usambazaji wa maji safi na malango 10 ya kukusanya mapato katika hifadhi za Taifa Ibanda-Kyerwa (1), Serengeti (2), Kilimanjaro (1), Tarangire (1), Ruaha (1), Katavi (1), Nyerere (1) na Mikumi (2).

“Pia, Shirika litajenga studio ya kurusha vivutio vya utalii mubashara itakayowezesha vivutio kurushwa moja kwa moja kwenye mitandao na chaneli za kimataifa,” amesema waziri huyo mwenye dhamana ya maliasili na utalii.

Wizara ya Maliasili na Utalii leo imewasilisha makadirio ya Bajeti ya jumla ya shilingi 654,668,208,000 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Kati ya fedha hizo, shilingi 486,501,449,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi 168,166,759,000 ni za miradi ya maendeleo.
Waziri Mchengerwa akionesha begi lenye nyaraka za hotuba ya bajeti kabla ya kuiwasilisha bungeni

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages