NEWS

Saturday, 4 July 2026

Musoma Mjini: Waziri Mkuu ataka uwekezaji uanze MUTEX kuchochea maendeleo



Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba (aliyevaa skafu) akipokewa katika Jimbo la Musoma Mjini kwa ziara yake ya kikazi jana.

Na Godfrey Marwa
Musoma
--------------

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ameelekeza serikali ya mkoa wa Mara na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakikisha kiwanda cha MUTEX kinaanza uwekezaji ili kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii mkoani humo.

Alitoa maelekezo hayo katika mkutano wa hadhara Julai 3, 2026 mjini Musoma, kufuatia ombi la Mbunge wa Jimbo la Musoma Mjini, Mgore Miraji, ambaye aliiomba serikali kusaidia kuweka msukumo uwekezaji uanze katika kiwanda hicho cha nguo.

"RC (Mkuu wa Mkoa) hakikisheni mnafanya kazi kwa karibu kwa kushirikiana na wizara husika kuhakikisha kiwanda cha MUTEX uwekezaji unaanza,” Dkt. Mwigulu alielekeza.

Aidha, aliielekeza ofisi ya Mkuu wa Mkoa kutenga shilingi milioni 750 ili kati ya hizo, milioni 500 zigharimie ukarabati wa Kituo cha Afya kikongwe cha Bweri, na milioni 250 zigharimie ujenzi wa kituo cha afya kata ya Buhare eneo la Mugaranjabo ili kuwasogezea wananchi huduma ya matibabu karibu.

Naye Mbunge Mgore aliiomba serikali kupitia Bunge kubadilisha sheria zisizo rafiki, ikiwemo ya utozaji faini kwa madereva pikipiki za abiria (bodaboda) badala ya kukamata vitendea kazi vyao.

"Bodaboda wana vilio vingi, naomba sheria muingalie vizuri wafanyiwe kama dereva wa gari - kulipa faini baada ya muda flani,” alisema.

Kwa upande mwingine, alitaja hatua ya Chuo cha Maendeleo ya Jamii Buhare kuanza kutoa stashahada kama moja ya mafanikio makubwa katika kipindi cha miezi saba tangu aingie bungeni.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages