NEWS

Saturday 8 July 2023

DED Rorya matatani kwa kudharau Mwenge wa UhuruKiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2023, Abdalla Shaib Kaim akikagua mradi wa maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya leo.

Na Mwandishi wa

Mara Online News
--------------------------

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim, ameeleza kusikitishwa na vitendo vya kiburi, jeuri na dharau vilivyooneshwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Abdul Omari Mtaka, wakati wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo.

“Kwa masikitiko makubwa tumeumwa [tumeumizwa] sana na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri yetu ya Rorya, kwanza ameonekana ni mtu ambaye ameonesha kiburi, na fedhuli na ujeuri kwa Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2023.

“Tayari amekosa kutoa ushirikiano kwa viongozi wakati wanaendelea kumhoji na kutafuta taarifa mbalimbali kwa ajili ya kujiridhisha juu ya uwepo wa ukaguzi wa miradi.

“Hivyo kwa dhati kabisa, kwa niaba ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2023, tumeenda katika mradi wa kwanza tunamuulizia DT (Mhasibu wa Wilaya) hayupo, Mkurugenzi Mtendaji anajibu majibu mabovu na kuonesha dharau kwetu.

“Tumeenda mradi wa pili Mkurugenzi Mtendaji hakuonesha ushirikiano na pia kajibu majibu ya jeuri na ufedhuli kwa Mwenge wa Uhuru,” amesema Kaim wakati wa ukaguzi wa miradi ya maendeleo wilayani Rorya, leo Julai 8, 2023.

Kutokana na hali hiyo, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, amesema anamwachia Rais Samia Suluhu Hassan mamlaka ya kumchukulia hatua DED Mtaka.

“Nadhani ninayezungumza kama Mwakilishi wa Mheshimiwa Rais tunamwachia mwenyewe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Daktari Samia Suluhu Hassan hatua za kinidhamu na kisheria dhidi ya mtu huyu wakati maafisa pia mtaendelea na kuchukua hatua.

“Tutambue Mwenge wa Uhuru ni itifaki ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo naendelea kusisitiza hakuna mamlaka ambayo ipo juu ya Mwenge wa Uhuru. Kiitifaki uwepo wa chombo hiki maana yake ni uwepo wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na sisi ni wawakilishi namba moja wa Mheshimiwa Rais kupitia itifaki yake muhimu,” amesema Kaim.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages