NEWS

Tuesday 25 July 2023

Kijana aandika kitabu cha Hekima ya Rais Samia, atia neno Mkataba wa Bandari, atamani kuteta na Mkuu wa Nchi



Kijana Abel Sonda akizungumza na Mara Online News
---------------------------------------------------
 
Na Christopher Gamaina
wa Mara Online News
------------------------------

ABEL Sonda, Mwandishi wa kitabu alichokipa jina la The Demo Political Wisdom of President Dr Samia Suluhu (Hekima ya Kisiasa na Kidemokrasia ya Rais Dkt Samia Suluhu), amefanyiwa mahojiano maalumu na Mara Online News, ambapo pamoja na mambo mengine, ameweka hadharani ujumbe wa kitabu hicho, maoni yake juu ya mkataba wa uwekezaji wa uendelezaji wa bandari Tanzania na tamanio lake kwa Rais Samia - kuelekea kukamilisha kitabu hicho.

Yafuatayo ndiyo mahojiano yenyewe - yaliyochukua muda wa dakika 40 hivi mjini Tarime, Mara leo:

Mwandishi:
Hongera ndugu Abel Sonda kwa ubunifu na kazi ya kuandika kitabu hicho, na moja kwa moja nikuulize; kitabu hicho kimebeba ujumbe gani hasa kwa kifupi?

Abel:
Asante ndugu mwandishi. Kwa kifupi ujumbe wa kitabu hiki ni kwamba hekima huzaa uongozi ulio bora na unaotekeleza matakwa ya wananchi, na hakuna jamii ambayo inaweza ikawa nzuri zaidi bila kuwa na uongozi ambao ndani yake hekima imetawala.

Mwandishi:
Ulitoa wapi wazo hilo, na ni nini hasa kilikusukuma kuandika kitabu hicho?

Abel:
Wazo la kitabu hiki liliniijia wakati Rais alikuwa katika ziara mkoani Geita, nafikiri ilikuwa siku yake ya kwanza kutangaza msamaha kwa watoto wa kike waliopata ujauzito wakiwa shuleni, ili sasa waweze kurudi shuleni baada ya kujifungua.

Nilijiuliza maswali mengi - kwanini aliweza kufanya hivyo, baadaye nikasema kama kiongozi anapaswa kusamehe watu wake, anapaswa kutoa nafasi ya pili kwa watu wake. Kwa sababu kipindi cha nyuma watoto hawa walitelekezwa, na siyo tu kutelekezwa - walipewa adhabu, naita ni adhabu kwa sababu walizuiwa kuendelea na masomo.

Lakini Mheshimiwa Rais Samia Suluhu [akimaanisha Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania] alikaa chini na kutafakari kwamba badala ya watoto hawa kuwa burden (mzigo) kwa jamii na Serikali - kwa nchi na kwa wazazi, akaamua kuwapa nafasi nyingine ili waweze kurudi shuleni.

Hili jambo lilinigusa kwa kweli, lilinigusa sana na ndipo nikaamua kuandika juu ya hilo. Kwa hiyo aliwarudisha shuleni kuwafanya kuwa asset (rasilimali) ya wakati ujao. Nikiangalia pia hata viongozi wakubwa waliowahi kufanya vibaya wakasamehewa - wakarudishwa kwenye system (mfumo) walifanya mambo makubwa.

Mfano, Apostle Paul (Mtume Paulo) alifanya makosa mengi sana, aliua wakristo wengi, aliua wacha Mungu wengi, lakini baadaye Mungu aliona kitu ndani yake - alimsamehe, alimrudisha. Na katika Agano Jipya, Paulo amefanya mambo mengi zaidi kuliko watu wengi.

Naamini watakuja kutokea watu wakubwa katika hii nchi, naamini watakuja kutokea watu ambao wataleta ufumbuzi wa matatizo makubwa kwenye hii nchi - ambao Rais Dkt Samia Suluhu amewasamehe, naamini hicho kitu.

Kwa sababu pia msamaha haumaanishi kwamba watu warudi wakaendelee kutenda maovu, msamaha unamaanisha to start a fresh (kuanza upya), kuanza maisha mapya na ukawe mtu mpya, kiumbe kipya, ufanye mambo makubwa zaidi, ndio maana ya msamaha. Hivyo naamini hivi karibuni tutashuhudia vitu vikubwa vikitoka miongoni mwa watu waliopewa msamaha na Rais Dkt Samia Suluhu.

Kwa hiyo hicho kilinivutia kukiandika, nikasema nitatafsiri hili tendo ambalo amelifanya Dkt Samia Suluhu ili viongozi wengine wajifunze kuwapa msamaha, au nafasi nyingine watu wanapokuwa wamekosa.

Mwandishi:
Kwanini uliamua kuandika kitabu hicho kwa lugha ya Kiingereza, na je, una mpango wa kukitafsiri kwa lugha ya Kiswahili inayotumiwa zaidi na Watanzania?

Abel:
Nilitumia lugha ya Kiingereza kwa sababu ninatamani kitabu hiki kitumike kwa ulimwengu mzima, kisomwe na kila mtu aweze kutambua jinsi gani hekima ilivyo lulu katika uongozi. Watambue hekima ya ku- nab gate the challenges and troubles (kutatua changamoto na matatizo).

Duniani watu wengi wanaongea Kiingereza ndio maana nimetumia lugha ya Kiingereza ili kufikisha ujumbe huu kwa hadhira yangu.

Kuhusu kutafsiriwa kwa Kiswahili, naam, kitafanyiwa huo mchakato wa kukiweka pia katika lugha ya Kiswahili. Na kama nilivyosema natamani kitabu hiki kila mtu aje akisome na kimletee manufaa kwa sababu hekima si tu katika uongozi wa nchi, hekima inafaa kutumika katika uongozi wa familia na taasisi mbalimbali. Kwa hiyo kitatafsiriwa ili kila mtu ajue hekima iliyokuwa katika uongozi wa Dkt Samia Suluhu.

Mwandishi:
Lengo lako kuu la kuandika kitabu hicho ni nini hasa?

Abel:
Lengo kuu ni kuwafikishia viongozi wengine ujumbe waweze kujua wisdom (hekima) inaweza kutumika vipi katika kuleta mabadiliko makubwa kiuchumi, kisiasa na kidemokrasia.

Lakini pia kwa vijana wanaotamani kuwa viongozi wazuri waweze kujifunza kupitia hekima iliyopo kwenye uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu. Hilo ndilo lengo langu kubwa la kuandika kitabu hiki.

Mwandishi:
Tukiweka kando suala la uandishi wa kitabu hicho, kwa kuwa wewe ni mfuatiliaji wa mambo ya Serikali nchini, sasa hivi kuna hili suala la mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji na uendelezaji wa bandari nchini - kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai kupitia Kampuni ya DP World. Unalitolea maoni gani?

Abel:
Jambo hili kwanza limeleta controversy (mabishano), limeleta mjadala mkubwa, lakini mimi huwa napenda kuanza kujihoji kwanza, napenda kufuatilia viongozi waliopita, maamuzi waliyofanya yalikuwaje, halafu baadaye ndio tutarudi kwenye mkataba wa DP World.

Nitakupa mfano; nani aliyem- support (aliyemuunga mkono) Rais Magufuli [Rais John Pombe Magufuli, mtangulizi wa Rais Samia] pale alipotaka ku- terminate (kusitisha) ile mikataba ya madini - ukiachilia mbali mawakili wa Serikali, hakuna. Nani aliyem- support Magufuli kipindi anaenda against the world (kinyume na msimamo wa dunia) kwenye issue ya Covid-19, na kuna watu mpaka walilaani kwamba huyu mtu anaenda kuiteketeza nchi.

Lakini mimi mwenyewe pia nilikuwa na mashaka juu ya uamuzi wake, I saw death (niliona kifo), lakini Rais Magufuli mwenyewe aliweza kuona opportunity (fursa).

Nini maana yangu kuweza kuongelea hivi vitu vyote; narudi kwenye kumaanisha sasa kwamba kama angejitokeza mtu ambaye anam- support Magufuli kipindi cha kuvunja ule mkataba wa madini na kwenye issue ya Covid-19, ilikuwa na maana gani, ilikuwa ni ku- strengthen (kuimarisha) ule utashi wa kisiasa wa Rais Magufuli. Jibu ni kwamba hakuna mtu aliyekuwa tayari kufanya hivyo.

Sasa tunarudi kwenye huu mkataba. Huu mkataba umekaa katika mfumo wa kisiasa zaidi. Ndiyo, ni jambo la msingi na nasisitiza watu waendelee kuuliza maswali ili tuweze kujadili masharti na mambo mengine ya msingi katika huu mkataba.

Lakini watu wengine wanachukulia jambo hili kama ni sehemu ya ku- strengthen political muscles zao (kuimarisha misuli yao ya kisiasa). Kwa hivyo ukiangalia issue hii imechukuliwa kisiasa zaidi, siyo kwa maslahi ya wananchi. Sasa kama itaenda kisiasa, tunaweza kukosa vitu vya msingi, na kwa sababu wananchi wengi wameshakuwa na wazo kwamba hii nchi inauzwa - mkataba siyo mzuri, vitu kama hivyo, wamelalia kwenye mentality (mtazamo) ya mkataba siyo mzuri.

Binafsi sijauona huo mkataba lakini issues za sheria unaweza ukafikiri umeielewa kumbe hujaielewa, na ndio maana mtu mwingine anaweza akaua lakini akajitokeza wakaili akamtetea na akashinda.

Lakini pia issues za mkataba ni trick (ujanja) na ni confidential (siri). Hivyo mawakili wa Serikali hawataweza ku- expose (kufichua) kila kitu kwa sababu waki- expose wale jamaa [akimaanisha Kampuni ya DP World] wanaweza kuona kwamba ahaa hapa hawa jamaa [Watanzania] ‘wanatupiga’.

Kwa hiyo naamini kabisa kuna vitu vingi vya msingi ambavyo vinalinufaisha taifa letu kwenye huo mkataba havijawa exposed (havijawekwa hadharani) na ni kwa sababu ya kulinda maslahi mapana ya nchi. Serikali yetu haitaweza ku- expose (kufichua) kila kitu. Mawakili wa Serikali kuna namna ambavyo wameutafsiri huo mkataba wakauona kwamba una maslahi makubwa kwa nchi.

Kwa hiyo jambo la msingi ni kwamba all in all (yote kwa yote), naamini Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu jambo hili atakuwa amelifuatilia kwa mapana zaidi kwa sababu I know the level of her wisdom (najua kiwango cha hekima yake), kama anaamini kwamba jambo hili lina faida, namuunga mkono.

Na kwa sababu bandari ina mchango mkubwa sana katika uchumi wa hii nchi, na kama litafanikiwa jambo hili, hakika nakwambia tunakwenda kuandika historia ya kuwa na Rais bora kuwahi kutokea nchini. Kwa hiyo I support her (namuunga mkono).

Lakini pia sikatishi tamaa Watanzania wanaouliza vipengele vya mkataba. So in that sense (hivyo kwa mantiki hiyo) naiunga mkono Serikali.

Mwandishi:
Inavyoonekana kuelekea mkataba huo wa bandari Kampuni ya DP World itakuwa mwekezaji pekee, hatakuwa na mshindani. Je, unadhani kwa hali hiyo kutakuwa na ufanisi bandarini?

Abel:
Ndugu mwandishi mimi sio profesa wa biashara lakini hiki ndicho ninachokijua; linapokuja suala la biashara huhitaji kushindana ili uweze kuleta ubora, na kwa sababu nchi nyingi zimekuwa na hiyo dhana ya ushindani kwamba ili ufanisi uwepo mpaka ushindani uwepo, ndio maana nchi nyingi za Kiafrika zimekuwa zikishindwa.

Biashara haifai kufanya competition (ushindani), kwanza neno competition mimi huwa nalitazama kama comparison (ulinganisho), yaani unajilinganisha na mtu bila hata kuangalia uwezo wako, matamanio yako na ujuzi wako.

Naamini Serikali yetu itakuwa ime- set standards (imweka viwango) kwamba tunataka tufike pale. Tunahitaji kufikia viwango tunavyotaka. Huhitaji kuwa na ushindani ili kufikia viwango, is a dream (ni ndoto), is a vision (ni maono), vision ndiyo inayoweza kukuongoza.

Kwa hiyo sitegemei kwamba kwa sababu huyo mtu [DP World] hana mshindani eti ufanisi unaweza usiwepo, hapana. Serikali ita- set, na naamini kwamba ime- set standards za kufikia lengo - ambazo huyo jamaa atazifikia. Hivyo hatuhitaji ushindani, tunahitaji ufanisi wa vitu, vitu vifanyike kwa standards (viwango).

Mwandishi:
Mwanzoni ulidokeza kuwa unatamani kukutana na Rais Samia. Kwanini, una nini hasa unachotaka kumwambia, kumuuliza, au kuzungumza naye?

Abel:
Naam, natamani kukutana naye kwa sababu kama nilivyosema kitabu nilichoandika kimebeba historia yake na nimeona amekuwa na hekima sana kwenye safari ya maisha yake mpaka hapo alipofika.

Hivyo natamani kukutana naye ili kusudi cha kwanza, niweze kukamilisha kitabu hiki kwa sababu kuna baadhi ya vitu siwezi nikaviingiza mpaka nisikie kutoka kwake. Kwa hiyo nahitaji taarifa kutoka kwake kusudi ziweze kuleta tija kwa watu wengine, viongozi wa kizazi kinachokuja.

Natamani nimuulize baadhi ya maswali kwamba je, kuna policies (sera) alizozibadilisha, zilileta matokeo gani, alivyoweza kupita vikwazo, ili hatimaye kitabu changu kiweze kukamilika na kuleta tija kwa vijana na viongozi wengine walio serikalini ambao wanahitaji hekima.

Mwandishi:
Kwa kuhitimisha mahojiano haya, una ujumbe gani kwa viongozi wetu, hususan juu ya masuala ya siasa na demokrasia?

Abel:
Ujumbe wangu ni kwamba cha kwanza, huwezi kuwa kiongozi ukakosa kukosolewa. Nimejaribu kufuatilia viongozi wakubwa wote - hakuna aliyewahi kuongoza bila kukosolewa, kupingwa, kudhihakiwa na hata kutukanwa, hakuna kiongozi wa hivyo tangu dunia iumbwe.

Mungu mwenyewe mpaka sasa hivi bado anapata shida na wanadamu, baadhi ya watu wanampinga na kumkejeli waziwazi, so criticism is normal when it comes to leadership (hivyo kukosolewa ni kitu cha kawaida linapokuja suala la uongozi).

Mtu asiyestahimili kukosolewa hafai kwa nafasi ya uongozi, so criticism and leadership goes together (hivyo uongozi na ukosoaji vinaenda pamoja). Huo ndio ujumbe wangu kwa viongozi wa Serikali na kisiasa.

Lakini pia every vision it must be tasted (kila maono lazima yajaribiwe). Kwa hiyo viongozi wanapaswa kuzoea ukosoaji na kila ukosoaji unapokuja unakufanya ujirekebishe na kujiimarisha.

Viongozi wasipokubali kukosolewa watajikuta wanapatwa na hasira, watatukana na mwisho wa siku watakosa kuaminiwa, na hatimaye wananchi watakuja kuwapa uongozi watu ambao siyo sahihi.

Kwa hiyo nawaomba viongozi wazoee kukubali kukosolewa, kukosolewa ni kitu cha kawaida kwa kiongozi, so that is my advise to them (hivyo huo ndio ushauri wangu kwao). Kwa yeyote mwenye maoni au ushauri naomba awasiliane nami kupitia simu namba 0767367421.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages