NEWS

Monday 24 July 2023

Viongozi Tarime Vijijini, Barrick North Mara wakubaliana kuheshimu kanuni mpya za CSRMbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara (aliyesimama kulia) akizungumza katika kikao hicho cha kujadili Kanuni mpya za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii, kilichofanyika mjini Tarime wiki iliyopita. Aliyesimama kushoto ni Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano Mgodi wa North Mara, Hermence Christopher.
---------------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU
-----------------------------------

VIONGOZI wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Halmashauri ya Wilaya na Jimbo la Tarime Vijijini wamekutana kujadili Kanuni mpya za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii za Mwaka 2023, kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo chini ya mpango wa Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR).

Kikao chao kilifanyika mjini Tarime, Julai 18, 2023 ambapo kilitawaliwa na hoja za umoja na ushirikiano katika uzingatiaji wa kanuni hizo wakati wa uibuaji na utekelezaji wa miradi inayogharimiwa na fedha za CSR.

Kanuni hizo zimeainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 409 la tarehe 23/6/2023, Sheria ya Madini, Sura ya 123, ambazo zimetengenezwa chini ya kifungu cha 129 na kuidhinishwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko, Juni 15, 2023.

Mpangilio wa kanuni hizo umegawanywa katika sehemu tano zenye vipengele mbalimbali, ikiwemo uundaji wa kamati ya wataalamu na majukumu yake, vipaumbele vya jamii zilizopo katika maeneo yenye shughuli za madini.

Pia ukaguzi na taarifa za fedha, usimamizi na ukaguzi wa utekelezaji wa mpango, utatuzi wa migogoro na uenezaji wa elimu kuhusu wajibu wa mmiliki wa lenseni ya madini.Aidha, sehemu ya pili ya kanuni hizo mpya, inataja wajibu wa mmiliki wa leseni ya madini kwa jamii kuwa ni pamoja na kutenga asilimia 40 ya fedha za CSR kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika vijiji vilivyo jirani na mgodi, na asilimia 60 kwa ajili ya miradi ya halmashauri ya wilaya.

Kabla ya kanuni hizo mpya, asilimia 100 ya fedha za CSR ilikuwa zinaelekezwa kwenye vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara, lakini msimu uliopita ilipunguzwa hadi asilimia 70, ambapo asilimia 30 ilielekezwa kwenye vijiji vyote visivyopakana na mgodi katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Akichangia mjadala, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles alitaka kuwepo na ushirikiano wa dhati kati ya viongozi wa Serikali, mgodi wa Barrick North Mara, jimbo, kata, vijiji na wananchi wa kawaida katika uzingatiaji wa kanuni hizo mpya ili kufanikisha utekelezaji wa miradi chini ya mpango wa CSR.

“Tuzingatie hizi kanuni, miradi itekelezwe kwa wakati. Tukiwa kitu kimoja hakuna kitakachoshindikana,” alisema Kiles ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nyakonga kwa tiketi ya chama tawala - CCM.

Mwenyekiti Kiles (kulia) akichangia hoja katika kikao hicho

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomon Shati aliunga mkono hoja ya ushirikiano katika uzingatiaji wa kanuni hizo na utekelezaji wa miradi, akidokeza kuwa miradi itakayopewa kipaumbele kipindi hiki ni pamoja na ya kimkakati.

“Sasa tunaenda kutekeleza miradi ya kimkakati itakayogusa vijiji vyote, hivyo ushirikishaji viongozi na wananchi kwa ujumla uwepo kuanzia ngazi ya chini. Tukishirikiana na kuwa wamoja miradi ya CSR itatekelezwa vizuri na kwa wakati,” alisema Shati.

Mkurugenzi Shati (katikati) akijenga hoja katika kikao hicho

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini kwa tiketi ya CCM, Mwita Waitara alisema “Naunga mkono hoja ya ushirikishaji, ni muhimu sana… Madiwani waelimishwe hizi kanuni mpya na tushirikiane kuzitekeleza, kwa sababu zisipotekelezwa itakuwa ni kuvunja sheria.”

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano Mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher alisema wamejipanga kuhakikisha kuwa viongozi na wananchi husika wanashirikishwa kikamilifu kwenye vikao vyote vinavyohusiana na miradi inayolengwa na fedha za CSR.

Lakini kwa upande mwingine, Christopher alisema bado mgodi wa Barrick North Mara utaendelea kutumia Kamati ya Maendeleo ya Jamii (CDC) katika shughuli mbalimbali kwa manufaa ya mgodi huo na jamii inayouzunguka.

“CDC ni muhimu kwetu sisi, hata Rais wa Barrick anapokuja anakutana na wajumbe wa CDC, hivyo tunaitumia kutatua changamoto balimbali katika jamii na mgodi, ikiwemo kuelimisha jamii kuepuka vitendo vya uhalifu mgodini,” alisema.


Sehemu ya washiriki wa kikao hicho katika picha ya pamoja

Kikao hicho cha kujadili Kanuni mpya za Wajibu wa Wamiliki wa Leseni za Madini kwa Jamii, kilihudhuriwa pia na Mtaalamu Mshauri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt Fred Okangi, Mwanasheria wa Barrick, Raymond Ngatuni, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Idara ya Mahusiano Barrick North Mara, Sarafani Msuya, Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Sheria wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Goodluck Lukandiza na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl Saul Mwaisenye, miongoni mwa viongozi wengine.

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages