NEWS

Monday 17 July 2023

Mbunge Waitara awapa tano watendaji Mgodi wa North Mara kwa usimamizi mzuri wa miradi ya CSR

Mbunge Mwita Waitara (kushoto mbele) akizungumza katika mkutano wa Rais na CEO wa Kampuni ya Barrick na viongozi mbalimbali wa kijamii kwenye ukumbi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, wiki iliyopita.
----------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
------------------------------------------

MBUNGE wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara amewapongeza watendaji wa Mgodi wa Dhahabu Barrick North Mara kwa usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa chini ya mpango wa Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR) wa Kampuni ya Barrick.

“Watendaji wa Barrick wapo mstari wa mbele kufuatulia na kuhakikisha kuwa miradi ya CSR inakidhi thamani ya pesa (value for money),” amesema Mbunge Waitara.

Alitoa pongezi hizo alipozungumza katika mkutano wa Rais na Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow na viongozi wa kijamii kutoka kata na vijijii vilivyo jirani na mgodi wa North Mara, uliohudhuriwa pia na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa mgodi huo, Jumatatu iliyopita.

Waitara alisema kampuni hiyo ya madini imetoa shilingi zaidi ya bilioni saba kwa ajili ya kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika jimbo hilo lenye ukwasi mkubwa wa madini.

Miradi inayopewa kipaumbele kupitia mpango wa CSR Barrick ipo kwenye maeneo matano; ambayo ni elimu, afya, usalama wa chakula, maji na uchumi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda aliushukuru mgodi wa Barrick North Mara kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kijamii na kiuchumi.


RC Mtanda akizungumza katika mkutano huo.

“Niwashukuru mgodi [Barrick North Mara] kwa namna mnavyochangia masuala ya maendeleo, sio Tarime tu hata maeneo mengine ya mkoa wa Mara, tutaendelea kushirikiana,” alisema RC Mtanda katika mutano huo ambao pia ulihudhuriwa na viongozi wengine wa serikali, akiwemo Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa.

Aidha, RC Mtanda alisema serikali itaendelea kuhakikisha kunakuwepo usalama wa kutosha kwa Kampuni ya Barrick, wafanyakazi wake na jamii inayoishi jirani na mgodi wa North Mara ambao umetoa ajira kwa mamia ya Watanzania.

“Niwahakikishie kuwa ulinzi na usalama wa Barrick utazingatiwa, na jambo la pili ni kutatua migogoro,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa wa Mara.

Aliongeza kuwa uimarishaji wa uhusiana kati mwekezaji wa Kampuni ya Barrick na wananchi utapewa kipaumbele.

Naye Rais na CEO wa Barrick, Bristow, alitumia nafasi hiyo kuelezea mafanikio ambayo migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu imepata tangu 2109 ilipochukua hatuamu ya kuiendesha kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.


Rais na CEO wa Barrick akifafanua jambo katika mkutano huo.

Bristow alisema Barrick inapanua mradi wa maji ambao umetekelezwa katika kijiji cha Nyangoto ili uweze kuhudumia vijiji vingine saba vinavyopakana na mgodi wa North Mara.

Mradi huo ambao ulizinduliwa rasmi Julai 6, 2023 na Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023, Abdalla Shaib Kaim, kwa sasa unahudumia wananchi takriban 35,000 katika vijiji vya Nyangoto, Mjini Kati, Matongo na Nyabichune.

Lakini sasa mpango uliopo ni kapanua mradi huo ili uweze kuhudumia vijiji vyote 11 ambavyo vipo jirani na mgodi huo.

Kwa mujibu wa Bristow, tayari ripoti ya kwanza ya mpango wa upanuzi wa mradi huo imeishaandaliwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kwa ajili maandalizi ya awali ya utekelezaji.

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages