NEWS

Wednesday 5 July 2023

Mtuhumiwa kinara wizi wa mawe yenye dhahabu mgodi wa Barrick North Mara afikishwa mahakamani, aunganishwa na wenzake 8 kesi ya uhujumu uchumiNa Mwandishi wa
Mara Online News
-------------------------

RAPHAEL Matiku Zacharia - maarufu kwa jina Rapha (30), amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Tarime, akishtakiwa pamoja na wenzake wanane katika Kesi Namba 10/2023 ya Uhujumu Uchumi yenye mashtaka manne, likiwemo la wizi wa mawe yenye dhahabu katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara Ltd.

Rapha ambaye anatajwa kuwa mfanyabiashara na mkazi wa Bweri katika Manispaa ya Musoma, amefikishwa katika mahakama hiyo leo Julai 5, 2023 kuunganishwa na washtakiwa wenzake wanane katika kesi hiyo.

Akisoma kesi hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Stanley Mwakihaba, Mwendesha Mashtaka Wakili wa Serikali, Dotto Banga akisaidiana na Mwendesha Mashtaka mwenzake Wakili wa Serikali, Filbert Boniphace Mafuru, amedai kuwa Rapha na wenzake wanane walitenda makosa yanayowakabili kwa nyakati tofauti kati ya Aprili 28 na Mei 8, 2023 katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara Ltd uliopo wilayani Tarime.

 

Wakili Banga amewataja washtakiwa wengine katika kesi hiyo kuwa ni Emmanuel Joseph Mwita “Stamina”(32), Ghati Mumuncha Bale (38), Hamis Michael Marco “Lucas Andrew Morani” (36), Chacha Kirindo Mwita (35), Mang’era Bina “Chacha” (40), Frank Dickson Nyaika (30), Abia Sasi “Mama Neema” (48) na Makenge Chacha Nyaisa (20).

Amedai kuwa katika shtaka la kwanza, Rapha anashtakiwa kuongoza kundi la uhalifu kinyume cha sheria. Kwamba kwa nyakati tofauti kati ya Aprili 28 na Mei 8, 2023 katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara Ltd, kwa makusudi washtakiwa wote tisa waliiba gramu 3,798.4 za mawe yenye madini ya dhahabu yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania 77,584,800.

Mwendesha Mashtaka huyo ametaja shtaka la pili linalowakabili washtakiwa hao kuwa ni kupatikana na madini hayo ndani ya mgodi huo bila vibali vya umiliki, uchimbaji na udalali.

Ametaja shtaka la tatu kuwa ni wizi wa gramu 3,798.4 za mawe yenye madini yenye thamani ya Shilingi za Kitanzania 77,584,800 na shtaka la nne ni utakatishaji fedha huku wakijua ni mapato ya kosa la wizi.

Katika kesi hiyo namba 10/2023 ya uhujumu uchumi, washtakiwa wote tisa wanatetewa na Wakili David Mwita, ambaye hata hivyo hakutakiwa kujibu chochote kutokana na mahakama hiyo kutokuwa na mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.

Hivyo Hakimu Mkazi Mwandamizi, Mwakihaba, ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 10, 2023 kwa ajili ya kusomwa mahakamani hapo dhidi ya washtakiwa wote tisa ambao wako rumande.


#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages