NEWS

Wednesday 19 July 2023

Mzabuni wa Barrick North Mara akabidhi msaada wa nyumba pacha ya walimu Sekondari ya Matongo



Makabidhiano na uzinduzi wa nyumba pacha (two in one) ya walimu katika Shule ya Sekondari Matongo iliyojengwa na Kampuni ya Swala Solutions.
--------------------------------------------------

Na Mwandishi wa

Mara Online News
-------------------------

KAMPUNI ya Swala Solutions ambayo ni mzabuni wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara imekabidhi msaada wa nyumba pacha (two in one) ya walimu kwa Shule ya Sekondari Matongo iliyopo Kaskazini Magharibi mwa mgodi huo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Makabidhiano hayo yamefanyika sambamba na uzinduzi rasmi wa nyumba hiyo katika hafla maalum iliyofanyika shuleni hapo leo Julai 19, 2023.

Akizungumza katika hafla hiyo, Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye amezishukuru kampuni za Swala Solutions na Barrick, akisema msaada wa nyumba hiyo umeipunguzia shule hiyo changamoto zinazoikabili.


"Tunamshukuru sana mdau wetu Swala. Nyumba hii ni nzuri sana na hata mkandarasi ameitendea haki. Nitoe shukrani nyingi pia kwa mgodi wa Barrick kwa kutusaidia kutatua changamoto na kwenye sekta ya elimu tunaenda vizuri sana," amesema Kegoye ambaye ndiye amekuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo.

Ameishukuru pia Serikali ya Kijiji cha Matongo na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kwa ushirikiano mkubwa waliouonesha katika kusimamia utekelezaji wa mradi huo wa elimu.


Kaimu Meneja Utekelezaji wa Kampuni ya Swala Solutions (kushoto) akikabidhi funguo za nyumba ya walimu kwa Diwani wa Kata ya Matongo, Godfrey Kegoye na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Daudi Itembe.
-----------------------------------------------------
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Matongo, Daudi Itembe amesema msaada huo ni ishara ya matunda ya mahusionao mazuri yaliyopo kati ya Kampuni ya Barrick na jamii inayozunguka mgodi huo.

“Barrick ni mdau mkubwa sana wa maendeleo katika kata ya Matongo na sioni tabu kusimama na kusema mgodi unafanya vizuri," amesem Itembe huku akitaja miradi mingi ambayo inatekelezwa katika kijiji hicho kwa ufadhili wa mgodi wa Barrick North Mara.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Eneo wa Kampuni ya Swala Solutions, Roy Kiprono Kimutai ameshukuru kwa ushirikiano walioupata kutoka Barrick North Mara, Serikali ya Kijiji, Kata ya Matongo na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime katika utekelezaji wa mradi huo.

Naye Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher ameipongeza Kampuni ya Swala Solutions, akisema kitendo walichofanya ni mfano wa kuigwa.

“Huu ni ushirikiano mzuri na kwenye vikao vyetu tunahamasisha wakandarasi/ wazabuni kutoa kidogo kwenye sehemu ya faida yao kurudisha kwenye maendeleo ya jamii,” amesema Christopher.

Ameongeza kuwa manufaa ya mgodi wa Barrack North Mara kwa jamii inayouzunguka ni makubwa, ikiwemo kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR).


Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano wa Barrick North Mara, Hermence Christopher (katikati) na Kaimu Meneja wa Idara ya Mazingira wa Mgodi huo, Alex Maengo (kulia) wakipokea cheti cha pongezi kutoka kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Matongo, Mwalimu Zabron Orege.
----------------------------------------------------
Awali, Mkuu wa Shule ya Sekondari Matongo, Mwalimu Zabron Orege amesema nyumba waliyokabidhiwa imefanya idadi ya nyumba za walimu zilizokamilika shuleni hapo kufikia nne, kila moja ikiwa pacha (two in one).

Mwalimu Orege amesema ujenzi wa nyumba za walimu nyingine mbili unaendelea, na kwamba shule hiyo ina walimu 12 (wanaume tisa na wanawake watatu) na wanafunzi 228.

Hafla ya makabidhiano hayo imehudhuriwa pia na viongozi wengine mbalimbali wa kijamii, wananchi wa kawaida na Mkurugenzi wa Nyamongo Contractors and Mine Company Ltd, Samwel Paul Bageni ambaye ameipatia shule hiyo msaada wa kompyuta mbili zenye thamani ya shilingi milioni tatu ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na mgodi wa Barrick North Mara katika kuinua sekta ya elimu katani Matongo.

Mgeni rasmi, Godfrey Kegoye akizungumza katika hafla hiyo.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages