NEWS

Monday 17 July 2023

Namba Tatu aibuka mkataba wa bandari, awanyooshea kidole wakosoaji wabaya wa Rais Samia, ataka viongozi wamsaidie kujibu hoja


Mwenyekiti Mstaafu wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye "Namba Tatu"
 ---------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

-------------------------------------

MWENYEKITI Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye - maarufu kwa jina la Namba Tatu, ameibuka na kuwanyooshea kidole watu wanaomkosoa vibaya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, kuhusu mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji na uendelezaji wa bandari nchini - kati ya Serikali ya Tanzania na ya Dubai.

“Watu wamheshimu Rais, wasimnyooshee vidole na kumsemasema vibaya, huyu ni Rais wa nchi, wanapomnyooshea vidole na kumsemasema vibaya kwa kweli sisi hatuoni vizuri,” alisema Namba Tatu katika mazungumzo na Sauti ya Mara mjini Tarime, jana.

Alisema wana-CCM na wananchi wanaoitakia mema Tanzania hawapendi kuona na kusikia Rais mwenye mamlaka ya nchi akikosewa heshima na watu wachache wasio na staha katika ukosoaji.

“Naomba wale wanaomnyooshea kidole Rais waache, wamheshimu, huyu ni Rais wa nchi mwenye mamlaka, wasimdhihaki Rais wetu, hatutakubali kuona Rais wetu anadhihakiwa, ananyooshewa kidole, anakashfiwa… Mambo ya bandari imekuwa hoja ya kumnyooshea Rais kidole kila siku, hatutakubali,” alisisitiza.

Kwa upande mwingine, Namba Tatu alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuwaomba viongozi wote wa CCM na Serikali kujitokeza kumsaidia Rais Samia kujibu hoja zinazoibuliwa kuhusiana na mkataba wa ushirikiano wa uwekezaji na uendelezaji wa bandari nchini.

“Viongozi wote wa CCM kuanzia ngazi ya tawi, kata, wilaya hadi taifa tumsaidie Rais kazi, tusimwache Rais ananyooshewa vidole na sisi tumekaa kimya, tusimwachie Rais hili suala la bandari peke yake.

“Naomba wasaidizi wa Rais, mawaziri, viongozi wa mkoa, wenyeviti, waenezi wa chama msaidieni Rais kusema, kuna masuala inatakiwa sisi ndio tujibu, sio kila kitu Rais ndiye aseme. Rais aliwaweka hapo ili mmsaidie, msimwache Rais anasemwa ninyi mmekaa kimya,” alisisitiza Namba Tatu.

Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages