NEWS

Monday, 23 February 2026

Bodi ya Tumbaku Tanzania mbioni kufungua ofisi Mara



Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Stanely Mnozya.

Na Mwandishi Wetu
Mara
-------------

Bodi ya Tumbaku Tanzania (TTB) ina mpango wa kufungua ofisi zake katika mkoa wa Mara, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Stanely Mnozya amesema.

Ofisi hizo zitasogeza huduma karibu na wakulima wa zao la tumbaku katika mkoa huo wa Kanda ya Ziwa.

“Tutafungua ofisi za TTB hapa mkoani Mara ili kufikisha huduma kwa wananchi,” Mnozya alisema wiki iliyopita katika mahojiano maalum na Gazeti la Sauti ya Mara wakati wa ziara yake ya kukagua masoko ya tumbaku mkoani Mara.

Makao Makuu ya Bodi ya Tumbaku Tanzania yapo mkoani Morogoro.

Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd) kimesema uamzi wa TTB wa kufungua ofisi zake Mara ni habari njema kwani itasaidia kuharakisha maedeleo ya zao hilo katika mkoa huo.

Mkurugenzi Mkuu wa TTB, Mnozya, alitumia fursa hiyo pia kuwaondoa wakulima hofu akionya kuwa Bodi hiyo haitasita kuchukua hatua kali dhidi ya kampuni zilizopewa leseni ya kununua tumbaku katika wilaya ya Serengeti ikiwa hazitatenda haki kwa wakulima.

“Natoa maelekezo kwa kampuni zote zinazonunua tumbaku hapa Mara zihakikishe zinatoa bei nzuri kwa wakulima,” Mnozya alisisitiza na kuongeza kuwa TTB itawanyang’aya leseni wanunuzi watakaojaribu kuwanyonya wakulima kwa kutoa bei ya chini kwa kisingizio cha bei ya tumbaku kushuka katika soko la dunia.

Mnozya alitaja kampuni ambazo zimepewa leseni ya kununua tumbaku katika wilaya ya Serengeti kuwa ni Alliance One na Global Leaf.

“Kamwe wasijifiche kwenye mwamvuli wa kushuka kwa bei ya tumbaku, Bodi haitasita kufuta leseni zao za ununuzi wa tumbaku. Kampuni zote zitende haki,” alisema kwa msisitizo.

Hivyo, Mnozya alitoa wito kwa wakulima wa wilayani Serengeti kuendelea kujitokeza kuuza tumbaku waliyovuna akisema bado kuna fursa ya kunufaika kwa kupata kipato kizuri.

“Ninawahamasisha wakulima kuendelea kupeleka tumbaku waliyovuna sokoni. Wanayo fursa ya kupata kipato kwa sababu hata dola imeimarika, lakini pia kwa hali ya hewa iliyopo hapa kwa sasa, tumbaku ina ubora mzuri,” alisema Mnozya.

Alisema hivi sasa, bei ya tumbaku kwa daraja la kwanza ni dola za Kimarekani 3.02, daraja la pili ni dola 3, huku wastani wa bei ukiwa dola 1.95 (sawa na shilingi 5,169) kwa kilo moja.

“Kampuni za Alliance One, Global Leaf zimepewa leseni kununua Tumbaku wilayani Serengeri, lakini tuna mpango wa kuleta mnunuzi mwingine kwa wilaya ya Butiama,” Mnozya alidokeza akiwa katika ofisi za WAMACU Ltd.

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi huyo Mkuu wa TTB pia alionya utoroshaji wa zao la tumbaku nje ya nchi akisema watakaokutwa wakifanya hivyo watakambuna na mkono wa sharia.

Alitoa wito kwa mamlaka mbalimbali za serikali kuunganisha nguvu kudhibiti utoroshaji wa zao hilo kwenda nje ya nchi kwa manufaa ya taifa.

“Viongozi wa serikali wakiwemo wakuu wa wilaya washirikishwe kuzuia utoroshaji wa tumbaku kwende nje ya nchi “, alisisitiza Mnozya.

Alisema vitendo vya utoroshaji wa tumbaku kweda nje ya nchi unalikosesha taifa mapato , hivyo unapaswa kudhibitiwa.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu (GM) wa WAMACU Ltd, Samwel Gisiboye, alimpongeza Mkurugenzi MKuu huyo wa TTB kwa kufanya ziara ya kikazi katika mkoa huo na kuahidi kuwa ushirika huo utaendelea kushirikiana na Bodi hiyo kwa ustawi wa maendeleo ya kilimo cha tumbaku na kuinua uchumi wa wakulima wa zao hilo la biashara.

GM Gisiboye alisema maandalizi yote muhimu kwa ajili ya ununuzi wa tumbaku kwa mwaka huu wa 2026 yamekamilika katika mkoa wa Mara.

“Kwanza ufunguzi wa masoko ulishafanyika katika wilaya ya Serengeti na tunaendelea kuhimiza wakulima kuendelea kuleta mitumba (robota za tumbaku) kwenye masoko,” alisema.

Hadi sasa, wilaya ya Serengeti inaongoza kwa uzalishaji wa zao la tumbaku katika mkoa wa Mara.

Tumbaku ni moja ya mazao yanayoongoza kuingiza fedha za kigeni kwa maendeleo ya taifa, kwa mujibu wa taarifa zilizopo.

Kwa mwaka huu, bei ya tumbaku imeshuka katika soko la dunia baada ya uzalishaji wa zao hilo kuongezeka zaidi duniani na hivyo kuwa na ziada zaidi ya mahitaji.

Taarifa zinasema uzalishaji wa tumbaku kwa mwaka jana (2025) ulifikia takribani tani bilioni 5.8 dhidi ya tani bilioni 5.2 ambazo ni mahitaji ya zao hilo kwa dunia nzima.

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages