NEWS

Tuesday 11 July 2023

Rais wa Barrick azungumza na wanahabari, viongozi wa kijamii, aanika mafanikio ya North Mara, Bulyanhulu

Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow (katikati) akizungumza mkutanoni jana. Kulia ni Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa na kushoto ni Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Dkt Melkiory Ngido.

Na Mwandishi wa
Mara Online News
-------------------------

RAIS na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow amesema mafanikio yaliyofikiwa katika migodi ya dhahabu ya North Mara na Bulyanhulu inayoendeshwa na kampuni hiyo kwa ubia na Serikali ya Tanzania, ni mfano wa kuigwa katika shughuli za uchimbaji madini, hususan katika nchi zinazoendelea.

Bristow aliyasema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari wakati wa mkutano maalumu uliofanyika kwenye ukumbi wa mgodi wa North Mara jana Julai 10, 2023, uliowashirikisha pia viongozi mbalimbali wa serikali na wananchi ngazi ya taifa, mkoa, wilaya, jimbo, tarafa, kata na vijiji.Alifafanua kuwa tangu Barrick ichukue jukumu la kusimamia migodi ya North Mara (uliopo Tarime mkoani Mara) na Bulyanhulu (uliopo Kahama mkoani Shinyanga) mwaka 2019, imefanikiwa kuisuka upya na kuiwezesha kuzalisha dhahabu kwa kiwango cha daraja la kwanza.

Kwa mujibu wa Bristow, Barrick ilikuta migodi hiyo ikiwa katika hali ya kuporomoka na kushimamisha shughuli zake kutokana na mzozo kati ya serikali na waendeshaji wa awali.“Tulitatua mzozo huo na kuanzisha Kampuni ya Twiga kama ubia wa kugawana faida za kiuchumi kwa uwiano wa 50:50 ambao pia Serikali ya Tanzania ina umiliki wa hisa wa asilimia 16 katika kila mgodi.

“Tuliifufua na kuisuka upya migodi hiyo ambayo sasa kwa ujumla wake inazalisha dhahabu kwa kiwango cha daraja la kwanza. Kwa maneno mengine, mgodi wenye hadhi hii ni mzalishaji ambaye anaweza kuzalisha angalau wakia 500,000 za dhahabu kila mwaka - kwa miaka zaidi ya 10 kwa gharama zinazokubalika katika tasnia hiyo.

“Uendeshaji huu wa shughuli umefanikiwa sana kiasi kwamba tangu Barrick inunue hisa kutoka kwa wanahisa wenye hisa chache, umechangia kiasi cha dola zaidi ya bilioni 2.8 katika uchumi wa Tanzania kupitia kodi, ushuru, magawio, mishahara na malipo kwa wasambazaji wa ndani,” alisema Bristow.

Aidha, alisema Barrick imejijengea utamaduni wa kufanya kazi kama mwanajamii, hali ambayo imesaidia kurejesha uhusiano mzuri na jamii zilizo jirani na migodi hiyo.

Bristow aliongeza kuwa Kampuni ya Twiga Minerals inayounganisha Barrick na Serikali ya Tanzania katika ubia wa kuendesha migodi ya North Mara na Bulyanhulu, imewekeza dola zaidi ya milioni 12.5 katika miradi ya kihistoria inayoibuliwa kwa ushirikiano na Kamati za Maendeleo ya Jamii (CDCs) zilizoanzishwa katika migodi hiyo ili kutoa huduma bora za afya, miundombinu ya elimu, maji ya kunywa na vyanzo mbadala vya mapato.

“Miongoni mwa miradi hiyo ni mfumo wa umwagiliaji ambao unatarajiwa kuboresha uzalishaji kwa kiasi kikubwa kwa wakulima wapatao 2,356,” alisema Rais na Mtendaji Mkuu huyo wa Kampuni ya Barrick.

Aliongeza kuwa Barrick-Twiga pia imeshatoa dola milioni 30 kwa ajili ya Programu ya Kusongesha Mbele Mustakabali wa Shule (Future Forward School programme).

“Kwa ushirikiano na serikali, programu hii itajenga vyumba vya madarasa 1,090 na miundombinu mingineyo katika shule 161 nchi nzima ili kuchukua wanafunzi 49,000 kati ya wanaokadiriwa kufikia 190,000 watakaoanza kidato cha tano Julai mwaka huu [2023]. Aidha, imeahidi kutoa dola milioni 40 kwa ajili ya kujenga barabara yenye urefu wa kilomita 73 kutoka Kahama kwenda Kakola,” alisema Bristow.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Juma Chikoka (kushoto) na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara wakifuatilia mada katika mkutano huo.

Kiuendeshaji, mkusanyiko huo wa migodi ya Twiga (Twiga Complex), Bristow alisema umeendelea kuwa na utendaji mzuri wa uzalishaji na kwamba uko mbioni kufikia mwongozo wake wa uzalishaji wa mwaka huu.

“Migodi yote miwili inazingatia sana suala la afya na usalama wa wafanyakazi wao, na mwezi Aprili, mgodi wa Bulyanhulu ulishinda Tuzo ya Mshindi wa Jumla wa Uzingatiaji wa Taratibu za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Tanzania kwa Mwaka 2023 katika kundi la Sekta ya Madini, na mgodi wa North Mara ulikuwa mshindi wa pili,” alisema.Kuhusu ajira, Bristow alisema Barrick ina sera ya kuweka kipaumbele cha ajira za ndani, ambapo katika Kampuni ya Twiga sera hiyo imewezesha kupatikana kwa nguvukazi ambayo ni Watanzania kwa asilimia 96, huku takriban nusu yao wakitoka katika jamii zilizo jirani na migodi ya kampuni hiyo.

Sambamba na hayo, alidokeza kuwa uchimbaji wa kupekecha katika mgodi wa North Mara unafanikiwa kuchukua nafasi katika hifadhi zilizopungukiwa au kuishiwa dhahabu kutokana na uchumbaji, ambapo jiwe la kwanza la dhahabu lilichimbwa katika chimbo jipya la mgodi wa Gena katika robo ya mwaka uliopita, na kwamba fursa zaidi za uchimbaji wa kupekecha zimebainika katika migodi yote miwili.“Barrick imedhamiria kupanua uendeshaji wa shughuli zake nchini Tanzania kutoka hapa kwenye kituo chetu kikuu. Kwa sasa tunaunganisha leseni muhimu za utafutaji madini nchini kwa nia ya kupanua hifadhi na rasilimali zetu zilizopo, pamoja na kugundua maeneo mapya yenye dhahabu yaliyo na hadhi ya kimataifa,” Bristow alihitimisha.

Mkutano huo ulihudhuiwa pia na Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu North Mara, Apolinary Lyambiko, huku baadhi ya viongozi wa serikali na wananchi waliouhudhuria wakiwa ni Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Juma Chikoka na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara, miongoni mwa wengine.

Viongozi hao waliahidi kuendeleza ushirikiano na Kampuni ya Barrick katika shughuli za uchimbaji madini, kwa manufaa ya wananchi wanaoishi jirani na mgodi wa North Mara na Watanzania kwa ujumla.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages